Vijana wawili wamekufa maji huku wengine watatu wakinusurika baada ya mtumbwi wao kuzama walipokuwa wakienda kupiga picha kwenye mawe yaliyopo katikati ya Ziwa Singida.
Tukio hilo limetokea Ijumaa mchana Desemba 22, 2023 kwa vijana wanne waliofika kwenye ziwa hilo na kukodi mtumbwi kwa ajili ya kwenda kupiga picha kwenye mawe hayo yaliyopo katikati ya ziwa umbali wa takriban mita 300 kutoka ufukweni.
Mawe hayo ni kivutio cha watu kwenda kupiga picha na hukodi mtumbwi kutoka kwa wavuvi kwa kuelewana bei ya kwenda na kurudi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutabihirwa alipopigiwa simu kuulizwa ajali hiyo ya mtumbwi, hakupatikanana.
Maiti hizo mbili zilipatikana jana baada ya takriban juhudi za siku tatu za kuwatafuta, zilizofanywa kwa ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida.
Mwandishi wetu alishuhudia uopoaji wa maiti zilizopatikana na kutambuliwa kwa majina ya Jabir Iddy (21) na Mikidadi Rajab (20).
Mama mzazi wa Jabir Iddy, Nusra Said aliyekuwepo eneo la tukio amesema Ijumaa mwanaye alitoka nyumbani kwenda mjini kwa ajili ya kununua mbegu na baada ya hapo hakuongea naye tena, lakini jioni ya siku hiyo alipigiwa simu na kuambiwa mwanaye amezama ziwani.
"Ni mwanangu niliongea naye Ijumaa baada ya hapo sijaongea naye tena, aliondoka kwenda mjini kununua mbegu jioni ndio nikapigiwa simu nikaambiwa mwanao kazama sijui kwenye bahari sijui ziwa," amesema Nusra.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Singida, Inspekta Trobi Kowinga aliyekuwepo eneo la tukio, alisema utafutaji wa miili hiyo umefanyika kwa siku tatu.
Amesema wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara juu ya kuchukua tahadhali kwenye maji na kuwataka watumiaji wa ziwa kuwa makini.
"Mara kadhaa tumekuwa tukitoa elimu ya tahadhali tunapofanya shughuli zetu kwenye maji, niwaombe kutumia vifaa vya tahadhali kwenye maji na kuongeza umakini ili tuepuke ajali kama hizi, leo tumewapoteza wenzetu" alisema Kowinga.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Naima Chondo aliyekuwepo eneo la tukio baada ya miili hiyo kupatikana, amewataka watumiaji wote wa ziwa hilo kuchukua tahadhali ikiwemo kuvaa makoti maalum ya usalama wanapokuwa kwenye maji na kuwa na wataalam pindi ajali ikitokea.
"Watumiaji wote wanaokuja kwenye ziwa hili, hakikisheni mnakuwa waangalifu na mnatumia vifaa vya usaidizi majini hizi ‘lifejackets’ na wataalam," amesema Naima.
Amesema ofisi ya Zimamoto Mkoa imetoa magari mawili kwa ajili ya kubeba miili ya marehemu huku Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ikitoa mkono wa pole wa Sh100,000 kwa wafiwa.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamesema vijana hao walifika eneo hilo Ijumaa mchana kati ya saa saba na saa nane na kukodi mtumbwi huo kwenda eneo la mawe kupiga picha.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao mtumbi wao ulipigwa na mawimbi na kusababisha kujaa maji, ikawa chanzo cha ajali hiyo.
0 Comments