Waraibu Wa Biashara Ya Mapenzi Walalamikia Mipira Inayotoka China ‘Inawafinya’

 NA MWANGI MUIRURI 


Kumezuka uhaba mkubwa wa mipira ya kondomu katika vyumba vya mapenzi nchini huku zingine kutoka Uchina zikilalamikiwa kuwa ndogo sana kuliko silaha za wapambe wa kiume.



Hizo za Kichina zimesutwa kuwa konde na fupi na zinaishia kuwabana hivyo basi kuathiri raha ya tendo.


“Serikali iwajibikie hili suala la uhaba wa kondomu kama la dharura. Ni suala nyeti la kiusalama na pia la kiuchumi. Ni hatari inayohusu magonjwa ambayo yanakodolea macho mamilioni ya watu hapa nchini,” akasema Bi Fridah Kagwiria ambaye hushirikisha masilahi ya watoaji huduma za mahaba Mashariki mwa Mlima Kenya.


Bi Kagwiria alisema kwamba kwa sasa uhaba ulioko katika mang’weni na pia kwa wanaotaka kupanga uzazi uko juu kiasi kwamba wengine wanajifunga makaratasi ya plastiki ili kuokoa hali, wengine wengi wakiamua kuweka imani yao kwa Mungu kwamba hata bila kinga mambo yataishia kuwa salama.


Mwanamume mmoja tuliyekumbana naye katika chumba kimoja Mji wa Karatina aliteta kwamba mnamo Desemba 8, 2023 alikabidhiwa kondomu iliyokuwa na maandishi ya Kichina “na ambayo ilikuwa nyembamba na fupi kuniliko ikiishia kunibana na hata kuchomoka nikiwa kwenye majukumu”.


Mwanamume huyo aliteta kwamba huenda serikali iko na mtazamo kwamba ikizua uhaba wa kondomu nchini basi huenda sekta ya ukahaba iangamie “lakini huko ni kujidanganya kwa kuwa hata wakati wa Yesu duniani bado ukahaba ulikuwa”.


Hali hii ya uhaba wa kondomu ilianza kuathiri nchi mwaka wa 2021 ambapo mabwanyenye wa ufisadi hasa waliokuwa katika taasisi ya usambazaji madawa ya kimatibabu nchini (Kemsa) waliripotiwa kuiba kondomu 1.1 milioni. Kondomu hizo zilikuwa zimetolewa na shirika la Uswizi la Global Fund kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.


Anayeshikilia wadhifa wa Mfalme wa kondomu barani Afrika Bw Stanley Ngara amesema kwamba mfumo wa ushuru ndani ya uagizaji wa bidhaa hiyo ndio umezua upungufu huo.


Alisema kwamba serikali inahitaji wadau wa kushirikiana nayo katika usambazaji kondomu lakini kwa sasa wengi wamejitoa kufuatia kuhitajika kulipa ushuru wa juu.


Aidha, Bw Ngara ameteta kwamba viongozi nchini wameshindwa au wamepuuza kulifanya suala la Kondomu kuwa mdahalo wa kitaifa.


Meneja wa uhamasisho katika shirika la Aids Healthcare Foundation (AHF-Kenya) Bi Faith Ndung’u amesema kwamba “makahaba nchini wanafaa kuwa makini sana katika uhaba huo wa Kondomu unaovuma nchini”.


Bi Ndung’u alisema kwamba ni lazima serikali itie bidii katika kuzima visa vya ufisadi ambao huwaelekeza maafisa kuiba hata kondomu.


Aliongeza kwamba kwa sasa serikali imeweka ushuru wa kiwango cha Shilingi kwa Shilingi katika kuagiza Kondomu na badala yake inafaa kuingia katika mkataba usio na ushuru ili kufanikisha juhudi za usambazaji.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE