Shinyanga. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Shinyanga, Grace Bizulu amewataka wajumbe wa baraza la umoja huo kuwajali waume zao kwa kuwapa haki ya tendo la ndoa.
Pia, amewataka wanawake hao kuwalinda watoto wao wasifanyiwe ukatili.
Bizulu amesema hayo leo Desemba 21 katika baraza la umoja huo Shinyanga Vijijini na kuongeza kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakilalamika kuwa hawapewi haki yao ya ndoa.
"Tunapowanyima tendo la ndoa waume zetu tunawasababishia waende kwa michepuko, hivyo tubadilike tuhakikishe tunalinda ndoa zetu ipasavyo, tukifanya hivyo tutapunguza kuwa na watoto wa mitaani.
"Niwaombe wanawake wenzangu msijisahau mkawatelekeza waume zenu, rudisheni upendo wa zamani na walindeni watoto wenu ili wasifanyiwe ukatili, ukiwa na kazi nyingi ukasahau kuzungumza na mtoto na kumuelekeza kwamba hiki ni kibaya atafanyiwa ukatili," amesema Bizulu.
Pia, amewataka wajumbe hao kujitambua na kufanya kazi zao za UWT kwa wakati huku wakiwaelekeza wajumbe wa matawi na kuelimishana pale ambako haelewi ili kuujenga umoja wa wanawake na chama.
"Niwasihi viongozi wangu mnapofanya kazi zenu mnatakiwa kusaidiana msisemane semane elekezaneni mshirikiane na madiwani wenu wa viti maalumu, pamoja na wabunge ili kuhakikisha mnasimama imara katika umoja wetu," amesema Bizulu.
Pia, amewataka kuanzisha vikundi kwa ajili ya manufaa yao na wanapotaka kukopa kwa ajili ya biashara wakope fedha kidogo kulingana na biashara zao wasikope nyingi wakashindwa kurejesha.
Katibu wa UWT Wilaya ya Shinyanga, Magdalena Dodoma amewataka wale ambao hawajalipa ada ya umoja huo, walipe kwa wakati na waendelee kujisajili na kuhamasisha wanawake kujiunga.
"Niwashukuru sana makatibu kwa kazi mnazozifanya, lakini niwaombe makatibu wote tutimize wajibu wetu kwenye majukumu yetu, kila mmoja ajue wajibu wake asisubiri kusukumwa,” amesema Dodoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake UWT Wilaya ya Shinyanga, Mektrida Kenuka amewataka wajumbe wakasimame imara katika kufanya kazi za jumuiya ya wanawake na maagizo yote walioagizwa wakayafanyie kazi.
Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga, Christina Mzava amewataka wajumbe wa baraza waunde ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) kwa kuanza kujichangisha Sh5,000 kwa mwezi, kwa kuwa kuna fursa ya kuwekeza hadi Sh20 milioni kisha waanze kukopeshana.
0 Comments