Nigeria. Majonzi yameendelea kutanda katika vijiji kadhaa vya Wilaya ya Bokkos, katikati mwa Taifa la Nigeria baada ya vifo kufikia 160 vinavyotokana na mfululizo wa mashambulizi ya magenge ya watu wenye silaha.
Viongozi wa jimbo la Plateau katika wilaya hiyo wamesema watu wenye silaha wamevamia vijiji takribani 20 na kushambulia na kuwauwa watu 113, kisha kuzichoma moto nyumba katika maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, hadi leo Desemba 26, 2023, idadi ya vifo imeongezeka kwa kasi kutoka watu 16 walioripotiwa Jumapili jioni katika eneo hilo lililokumbwa na mivutano ya kidini na kikabila kwa miaka kadhaa.
“Tumewakuta watu zaidi ya 300 wamejeruhiwa," amesema Monday Kasah, kiongozi wa Wilaya ya Bokkos alipozungumza na Shirika la Habari la AFP.
Kasah amesema wote wamepelekwa hospitali za wilaya hiyo, wengine kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Jos na wengine kwenye Wilaya jirani ya Barkin Ladi.
Katika Wilaya ya Barkin Ladi, wengine takribani 50 wameuwawa katika mashambulizi hayo
"Takriban watu 113 wamethibitishwa kuuawa, huku uhasama wa Jumamosi ukiendelea hadi alfajiri ya Jumatatu (jana)," amesema Kassah, ameliambia AFP.
Takwimu hizo zimewekwa wazi na mbunge wa jimbo, Dickson Chollom aliyelaani mashambulizi hayo, huku akitoa rai kwa vyombo vya usalama kuchukua hatua dhidi ya makundi hayo.
"Hatujakata tamaa katika mbinu za makundi hayo, tuko imara kwenye kutafuta haki na amani ya kudumu," amesema Chollom.
Gavana wa jimbo la Plateau, Caleb Mutfwang naye amelaani mauaji hayo akiyataja kuwa ya "kinyama na udhalimu mkubwa."
Jimbo la Plateau limekuwa na migogoro ya mara kwa mara baina ya jamii ya wafugaji ambao wengi ni Waislamu dhidi ya Wakristo wanaoendesha shughuli za kilimo.
Vyombo mbalimbali vya kimataifa vimenukuliwa vikieleza mauaji hayo huenda yamechochewa na chuki za kidini au kikabila.
Gavana Mutfwang amesema Serikali itachukua hatua za mapema kuzuia tukio hilo kutokea tena.
Hadi jana Jumatatu, milio ya risasi imeendelea kusikika, huku Mkazi wa kijiji cha Mushu ameliambia AFP kwamba Jumapili wamesikia mashambuzi kuuwa, kujeruhi baadhi na kuwateka nyara baadhi yao.
0 Comments