Benchi jipya la ufundi la Simba chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha limedhamiria kufanya mambo makubwa mawili ili kuendeleza heshima iliyoijenga timu hiyo pamoja na mafanikio ya uwanjani.
Benchikha na wasaidizi wake kwao suala la nidhamu siyo ombi ni amri inayotakiwa kutekelezwa na wachezaji wote bila kulazimishwa na inaelezwa wapo baadhi ya nyota ambao ameanza kuwanyoosha, huku jingine likiwa ni lile la wachezaji kupambana ipasavyo uwanjani kila wanapopata nafasi.
Katika suala la nidhamu kocha huyo ameanza na Clatous Chama na Nassor Kapama ambao wamesimamishwa kwa muda usiojulikana, huku chanzo ikielezwa ni suala la utovuni wa nidhamu.
Juzi jioni Simba ilitoa taarifa kuwasimamisha wachezaji hao kwa madai ya utovu wa nidhamu na pia kuwakumbusha watumishi wengine ndani ya klabu hiyo kuzingatia hilo, ili kila mtu atekeleze wajibu kama anavyotakiwa.
Hata hivyo, imebainika chanzo kilichowaponza wachezaji hao ni mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Wydad Casablanca ya Morocco ambapo timu hiyo ilishinda kwa mabao 2-0 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa mujibu wa chanzo kutoka Simba, inaelezwa kwamba katika mchezo huo Chama alitofautiana na kocha wa viungo, Kamal Boudjenane ambapo mkufunzi huyo aliripoti kwa Benchikha ambaye alionyesha rangi yake kwenye suala na nidhamu kwa kuukomalia uongozi kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya nyota huyo aliyedumu Msimbazi kwa misimu mitano akitumikia mitatu katika awali ya kwanza na miwili ile ya pili.
“Kocha wa viungo alimshitaki Chama kwa kocha mkuu kwamba alikuwa anabishana naye wakati anampa maelekezo ya kufanyia kazi uwanjani, jambo ambalo lilimchefua Benchikha na kumtaka mchezaji aombe radhi,” kilisema chanzo kutoka ndani ya Simba.
“Chama aligoma kufanya hivyo, kwani alikuwa na utetezi wake. Hata hivyo hatua ya kukataa kuomba radhi haikumzuia kocha kuwaomba viongozi wampeleke Kamati ya Nidhamu na kuwatangazia wachezaji wengine kutambua hakuna aliye juu ya Simba wanafanya kazi na wanalipwa, hivyo lazima wazingatie nidhamu inavyopaswa na wawe wazalendo kwa timu,” kilisema chanzo hicho.
“Mbaya zaidi kocha alisisitiza asiposhughulikiwa Chama atabeba mizigo yake ataondoka, kwani hayupo tayari kufanya kazi na wanaotaka kunyenyekewa anahitaji wanaojituma kwa ajili ya timu na kilichowakutanisha ni kazi na siyo jambo lingine.”
Juhudi za Mwananchi kumpata Chama jana kuzungumzia sakata hilo hazikuzaa matunda.
Ishu ya Kapama
Kuhusu kilichosababisha kiungo wa timu hiyo, Kapama kusimamishwa chanzo chetu kilieleza kuwa: “Kwa upande wa Kapama (kocha) ameona ni mchezaji aliye na dharura za mara kwa mara alizoziona ndani yake zina utegevu, hivyo akaona ni mtu anayehitaji kumuacha afanye kazi anazoona zinafaa, kwani ndani ya kikosi chake anahitaji washindani wa namba na kila mtu anampa nafasi aonyeshe alicho nacho.”
Hata hivyo, akizungumza na kituo cha redio cah EFM jana, Kapama alisema tuhuma zinazoelekelezwa kwake hazijui, lakini anachukulia suala hilo ni changamoto mahala pa kazi na litamalizika vizuri.
“Hayo yanayosemwa kwenye mitandao ya kijamii ni hisia tu ambazo si za kweli,” alisema Kapama.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa mkataba wa Chama unamalizika mwisho wa msimu huu, hivyo kama hatajirekebisha mbele ya Benchikha unaweza kuwa mwisho wake kikosini, huku Kapama ambaye hapati nafasi mlango wa kuondoka upo wazi.
Ukiachana na wawili hao, Luis Miquissone pia anatajwa kuchunguzwa mwenendo wake kwani kocha hataki wachezaji wenye majina makubwa wanaoishia kuvimba kutokana na historia ya kile walichofanya miaka nyuma klabuni hapo.
Badala yake kwa mujibu wa chanzo ni kuwa, Benchikha anataka watu wa kazi watakaofanya Simba inyakue mataji mengi zaidi ndani na nje.
Katika msisitizo wa nidhamu kikosini inaelezwa kwamba kuna nyota mwingine amekatwa mshahara kutokana na kuchelewa kufika mazoezini, jambo linalowafanya wengine kuanza kunyooka wakiamini kwamba wamepata kocha asiyependa utani na kazi.
Phiri ambao kuachwa
Taarifa zilizopatikana jana zilisema mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri ameomba kuachwa dirisha hili la usajili.
Hata hivyo, hakukuwa na upande uliothibitisha taarifa za nyota huyo Mzambia asiye na uhakika wa namba kuomba kuondoka, lakini kwa muda mrefu amekuwa haanzi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
0 Comments