Kenya, Tanzania na Uganda zilivutia zaidi ya dola bilioni 13.3 za uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) mwaka 2022, na kuzisaidia kubuni maelfu ya ajira mpya.
Ripoti ya hivi punde ya uwekezaji ya kampuni ya ushauri ya biashara ya Ernst & Young inaonyesha kuwa Uganda ilirekodi kiwango cha juu cha uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni ambapo ilivutia dola bilioni 10.2 - ambacho ni kiwango cha juu zaidi katika Afrika Mashariki - na kubuni nafasi za kazi 6,300.
Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini Kenya uliongezeka kwa asilimia 117 mwaka jana, na kuleta dola bilioni 2 na kuzalisha ajira 7,819, huku uwekezaji mwingi ukienda katika sekta za huduma za biashara, teknolojia, uchukuzi na maghala.
Nchini Tanzania, uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni ulipanda kwa asilimia 133 kufikia viwango vya kabla ya Covid-19, ambapo kuna miradi 21 yenye thamani ya dola bilioni 1.3 na kutengeneza nafasi za kazi 4,566.
Uwekezaji muhimu nchini Tanzania ni pamoja na ule wa shirika la Intracom lenye makao yake makuu Burundi, ambayo inapanga kujenga kiwanda cha saruji cha dola milioni 250 katika mkoa wa Kigoma ili kusambaza saruji katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, unaoshirikisha Tanzania, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Kenya (KenGen) pia inatarajia kuwekeza katika miradi miwili ya umeme wa jotoardhi nchini Tanzania.
Takwimu za Rwanda, Burundi na Sudan Kusini hazikupatikana, lakini nchini Ethiopia, uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni umepungua sana katika miaka mitatu iliyopita.
Ripoti hiyo ilisema kwamba "Kenya ndiyo nchi inayovutia miradi mingi zaidi Afrika Mashariki, huku Uganda ilipata mtaji mkubwa zaidi kupitia uwekezaji kutoka Ufaransa katika sekta ya mafuta na gesi."
0 Comments