Dodoma/Dar. Mjadala umeibuka kufuatia watoto kugombea nafasi za kisiasa, huku wasomi, wanasiasa, wanasaikolojia wakitofautiana maoni.
Hilo linatokana na uchaguzi wa kuwania nafasi za uongozi wa Chipukizi ndani ya CCM uliomalizika juzi.
Hoja ya wanaopinga watoto kuingia kwenye siasa, wanadai ni kutengeneza makundi ndani ya jamii, hivyo waachwe, ni mapema kuingizwa kwenye siasa.
Wasiwasi wa wanaopinga hali hiyo, ni baada ya kuona watoto wa vigogo walio madarakani wakigombea nafasi za uongozi, huku hofu ikiwa ni tabaka lililo madarakani kujiimarisha zaidi.
Hata hivyo, wapo wanaoona hoja hizo hazina mashiko kwa kuwa kiongozi anaanza kutengenezwa akiwa mdogo, hivyo ni muhimu vijana wenye mwelekeo waungwe mkono, wakisisitiza hakuna sheria inayokataza.
Kauli hizo zinakuja siku mbili tangu kutangazwa kwa safu mpya ya uongozi wa Chipukizi ndani ya UVCCM.
Kwenye uchaguzi huo, mtoto wa msanii Nurdin Bilal maarufu kama 'Shetta,' Qayllah Nurdin Bilal alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chipukizi CCM Taifa kwa kura 303, huku mshindani wake wa karibu, Hytham Mwanyemba akipata kura 96.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Atka Hassan Juma kura 372.
Nafasi za wajumbe wa kuwakilishi mikutano ya UVCCM zilikwenda kwa Isack Nchemba (Mjumbe wa Baraza kuu la UVCCM- Bara), Aiman Mohammed Baraza kuu la UVCCM-Zanzibar.
Uwakilishi wa nafasi ya ujumbe wa kamati ya uendeshaji Taifa kundi la wanawake alishinda Briana Mahiga aliyepata kura 151, wakati kundi la wanaume akichukua Simba Jerry Silaa aliyepata kura 155.
Madaraka akosoa
Madaraka Nyerere, mtoto wa Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Nyerere, akizungumzia uchaguzi huo, alisema ni vyema watoto wakaachwa hadi pale watakapofikisha umri wa kupiga kura ndipo wahusishwe kwenye siasa.
“Kuna umuhimu wa utoto, kwa nini uwaletee watoto presha, hujaona video ya watoto wakilia eti tu kwa sababu Simba au Yanga imefungwa? Mfano kwa hawa watoto walioshindwa uchaguzi utakuta wanalia kwa sababu tu ya kushindwa uchaguzi kama walivyo wale wa mpira,” alisema.
Alisema hana uhakika kama mambo ya kuwaingiza watoto kwenye uchaguzi hadi ngazi ya taifa yamewahi kutokea nchini.
Hoja ya Madaraka inafafana na ya Katibu Mkuu wa Chama Cha ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, aliyesema chama hicho hakiamini katika ushirikishaji wa watoto kwenye mifumo ya vyama vya kisiasa.
“Hatari yake ni kuwaingiza watoto kwenye hisia za ushindani na uhasama wa kisiasa, Uganda inaendesha programu za kuwajengea watoto uzalendo wa kupenda Taifa lao, sisi tunawajengea misingi ya vyama, ni hatari sana...” alisema Shaibu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara Anamringi Macha alisema watoto hao wanafundishwa msingi wa kuchaguana.
“Tunawaweka kwenye misingi, mfano mtoto wakati mwingine ukitaka awe msafi unaanza kumpa kitambaa afue na sio suruali,” alisema Macha ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa CCM.
Imeandikwa na Mainda Mhando, Baraka Loshilaa, Tuzo Mapunda na Kelvin Matandiko.
Akizungumzia kitendo hicho, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema walipoandika Katiba ya chama mwaka 2006, waliingiza kwenye Katiba suala la kuwa na muundo wa watoto wa miaka 12 – 17, siyo kama wanachama, bali kama wafuasi.
Alisema lengo lilikuwa ni kutengeneza chemchem ya uongozi ndani ya chama na siyo kuwalisha watoto itikadi kali za kisiasa ambazo zitaathiri malezi na makuzi yao, lakini watoto kukuzwa kwenye vipawa vya uongozi.
“Kwa hili lililofanywa na CCM, kauli zangu kama mtendaji mkuu wa chama ni mbili; kwanza, Msajili wa vyama vya siasa ajitokeze, aueleze umma iwapo hicho kilichofanywa na CCM ni halali kwa mujibu wa sheria na marekebisho ya sheria ya mwaka 2019.
“Pili, ninaelekeza Baraza la Vijana la Chadema ambalo tuliwapa wajibu wa kuwa walezi wa watoto kiuongozi, kutengeneza chemchem ya kukuza uongozi kwa wafuasi wa chama kati ya miaka 12 – 17, lirejee na kuanza kuruhusu chemchem waanze kububujika,” alisema.
Hakuna kosa lililofanyika
Majibu ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza hakuna sheria inayokata isipokuwa hao ni watoto na wala si wanachama kwahiyo wanaanza kulelewa kwenye misingi ya vyama.
"Hakuna sheria inayokataza isipokuwa hawa ni watoto hawana chama na wanaanza kulelewa katika mazingira ya kichama," alisema Nyahoza.
Kwa upande wake, Dk Tumaini Sanga, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John Tanzania alisema ni haki watoto wa matabaka yote kuingia kwenye siasa hata wakiwa ni viongozi ikiwa wana utashi, vipaji au nia ya kuwa viongozi wa baadae.
“Uongozi ngazi ya chipukizi haumbani mwananchi kutopeleka watoto wake kugombea nafasi za uongozi hivyo jamii iondoe hofu juu ya watoto wa vigogo,”alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema hakuna dhambi kwa watoto kuingia kwenye siasa au mtoto wa kiongozi kugombea nafasi yeyote na kupata.
Hakuna dhambi yeyote ya watoto hao kugombea nafasi na kupata, changamoto kuna watoto wengi ambao hawawezi kupata taarifa sahihi na wazazi wao hawana uelewa mpana wa masuala ya siasa, kwahiyo kunaonekana watu wale wale kupeana madaraka
Dk Loisulie alisema tafsiri iliyoibua mjadala ni tabaka linalotawala kujiimarisha kuendelea kubaki madarakani jambo ambalo ni wasiwasi ambao unaeleweka.
“Wale ambao hawajabahatika kuingia kwenye nafasi za uongozi hawatakaa kusogelea nafasi za uongozi ndio wasiwasi uliopo,” alisema
Kwa upande wake msaikolojia John Amrose alisema siasa nisuala la kijamii hivyo hakuna shida mtoto kujihusisha nayo.
“Siasa ni suala la kijamii ambalo mtu anakuzwa nayo kwa kujua malengo, utendaji na wajibu,jambo linaloleta shida ni wale tunaowaona wanazaliwa na viongozi waliopo madarakani ambalo kisaikoolojia ikunakuzwa kuona uongozi si kwa jamii yetu bali ni kwa mtoto wa fulani, kunakuwa kama ufalme wenye mihimili fulani,
“Kwahiyo otukiwa na chipukizi wanaotokana na viongozi ambao tayari wapo madarakani ni shida kubwa kwa baadae,” alisema.
Imeandikwa na Mainda Mhando (Dodoma), Baraka Loshilaa na Tuzo Mapunda na Kelvin Matandiko (Dar)
0 Comments