TUZO ZA FILAMU 2023: Sasa tunajitambua, ubora umeongezeka

 

UTOAJI wa Tuzo za Filamu za Tanzania (TaFFA), hufanyika kila mwaka kuanzia mwaka 2021 zilipoanzishwa kusherehekea mafanikio ya tasnia ya filamu nchini Tanzania.


Tuzo hizo zilianzishwa na Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) katika kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha programu zinazotambua, kutangaza na kuendeleza vipaji vya wasanii.


Nia ya serikali kuanzisha programu hiyo ambapo wadau wa sekta ya filamu Tanzania wanaofanya vizuri zaidi kwenye maeneo yao ya ubobevu hutunukiwa Tuzo na Serikali, ni kutambua mchango wao, kutambua vipaji vyao, kuwaongezea hamasa ya kuzalisha kazi nyingi zaidi za filamu, kuwaongezea hamasa ya kuzalisha kazi zenye ubora zaidi ili wawe na

ushindani mkubwa ndani na nje ya nchi, na kuibua fursa za uwekezaji katika eneo hilo.


Agosti 11, 2023 serikali kupitia Bodi ya Filamu ilifungua rasmi dirisha la upokeaji wa filamu kwa ajili ya Tuzo za Filamu Msimu wa Tatu wa Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania 2023 (Tanzania Film Festival Awards 2023 – TaFFA).


Kamati ya Sekretarieti ya Tuzo za Filamu inayoundwa na maofisa filamu kutoka Bodi ya Filamu, watendaji pamoja na wadau mbalimbali wa filamu ilifika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kupokea filamu zitakazowania tuzo.


Aidha, Tamasha la Tuzo la Filamu 2023 limetanua wigo na kuanzisha Kipengele kipya cha filamu za lugha ya Kiswahili kutoka Nchi za Afrika Mashariki.


Jumla ya filamu 565  ilipokelewa kwa nia ya kushiriki katika vipengele vya Tuzo za mwaka 2023 ambapo filamu 535 zimetoka Tanzania na filamu 30 kutoka nje ya Tanzania katika Nchi za Kenya, Uganda na DRC.


Baada ya zoezi la ukusanyaji wa filamu hizo kukamilika, lilifuatiwa na zoezi la uchambuzi wa filamu ambapo zilipatikana filamu 204 kutoka kwenye filamu za Tanzania na filamu zote 30 za Kipengele cha Afrika Mashariki.


Kama ilivyokuwa katika misimu miwili iliyopita, filamu zilizochaguliwa zilioneshwa kwenye Kituo cha Televisheni cha Azam Media kupitia Chaneli ya Sinema Zetu, Na. 103. Lakini pia

ilitolewa fursa kwa mwandazi wa filamu iliyochaguliwa kuamua ikaoneshwe katika televisheni gani nyingine nje ya Azam Media.


Pamoja na mambo mengine, Tamasha la Tuzo za Filamu 2023 ambalo lilifanyika Mlimani City Desemba 16, limeboreshwa katika maeneo sita ya kiutendaji, hususani kwenye eneo la ubora wa Tamasha la Tuzo.


Awali yote idadi ya filamu zilizopita mchujo wa awali ni kubwa zaidi kulinganisha na miaka ya nyuma. Mwaka jana jumla ya filamu 189 zilipita mchujo kati ya filamu 840 zilizopokelewa.


Lakini mwaka huu jumla ya filamu 204 zilifaulu katika hatua ya awali kati ya filamu 565 zilizopokelewa.


Kitakwimu, mwaka huu 41% ya filamu zilizopokelewa zimefaulu, ikiwa ni ongezeko la 18% kutoka 23% ya filamu zilizofaulu mwaka jana. Na hii inaleta maana kubwa zaidi kwamba waliowakilisha kazi zao walikuwa wanajiamini na kazi zimeboreshwa zaidi kutoka msimu uliopita.


Aidha, mwaka huu kitakwimu tu utaona kwamba kuna ukuaji katika tamasha kwani, Tuzo

zimefungua milango ya filamu za Kimataifa (Afrika Mashariki), ambapo kuna vipengele vya

filamu ndefu bora za Kiswahili na Tamthilia Bora za Kiswahili na uoneshaji wa filamu kuwa huru kwa kituo chochote kitakachoweza kuonesha filamu hizo badala ya Azam pekee kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita ya 2021 na 2022.


Tuzo za Filamu Tanzania ambazo zimegawanyika katika vipengele vingi, ikiwa ni pamoja na

filamu bora ya mwaka, Mwigizaji bora wa kike, Mwigizaji bora wa kiume, Mkurugenzi bora, Mtayarishaji bora, Mhariri bora, Mpiga picha bora, Mwanaanga bora, Muigizaji bora chipukizi, Filamu bora ya Afrika Mashariki hutolewa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali,

ikiwa ni pamoja na ubora wa uigizaji, uandishi, na uongozi.


Tuzo hizo ambazo ni muhimu kwa kuhamasisha ubora wa tasnia ya filamu nchini Tanzania

zimeibua filamu ya Jungwa kama mshindi wa jumla. Jungwa ni hadithi ya kusadikika

ikishaidisha uwezo na ubunifu mkubwa wa mtengenezaji filamu machachari na bora, Ben Royal.


Hii filamu kutoka Mkoa wa Mbeya na ni mwendelezo wa filamu za kusisimua na zenye ubora wa utambaji toka mkoa huo. Mwaka 2021 wakati tuzo zinaanza kulikuwapo na filamu ya Janga ya mtengenezaji huyo huyo Ben Royal akishirikiana na John Kokolo.


Ilikuwa ni filamu ambayo ilikuwa inahusu tatizo la maji ambalo ni suala mtambuka duniani.

Mwaka 2022 kutoka Mbeya pia kulikuwa na filamu ya Wandongwa ya John Kokolo. Ni filamu

iliyostaajabisha kwa utambaji wa hadithi zilizo tofauti na matarajio ya filamu toka Tanzania.


Filamu inayozungumzia jadi za kale mbaya na nzuri lakini za kufikirika, ikiongezea utamu kwa kuwa na sehemu kadha za kuchekesha na nyingine za kusikitisha. Kiuandishi ni filamu iliyotimia japo kulikuwa na vikosakosa vidogo.


Mmoja wa washiriki wa Tamasha la mwaka huu anasema kwamba anamkubali Ben Royal

kwani kwa mara nyingine tena ametengeneza filamu ya kisasa, ya kusadikika ambayo itaweza kabisa kuuzika kwenye majumba ya sinema kama itasaidiwa kimkakati.


Kwa misimu mitatu wahakiki wa sinema akiwemo Beda Msimbe wanasema kunaonekana juhudi za wazi za kukuza tasnia kupitia tuzo.


“Sasa tunaona filamu ambazo zinaweza kabisa kushindana kimataifa. La maana tasnia ianze kujitazama na kuwa na mikakati ya ukuzaji na uendelezaji bila kuogopa gharama,” anasema.


Profesa Martin Mhando, Mtaalamu na mwalimu wa masuala ya sinema anasema Tanzania kwa sasa ni dhahiri imefikia mahali ambapo lazima uwekezaji mkubwa ufanyike ili kuvuka korongo lililopo mbele ya tasnia ya filamu ya Tanzania.


“Lazima hapa serikali, wadau na wawekezaji kulitazama hili kwa macho makavu ya asubuhi ili tuweze kujenga tasnia endelevu ya filamu hapa Tanzania,” anasema Profesa Mhando.


Mmoja wa watu wa ndani katika mchujo anasema kwamba mwaka huu wametazama filamu

na picha za video zenye ubora wa kutia moyo. Na wamekutana na tamthilia ambazo Tanzania inaweza kujivunia kwa jinsi zilivyobuniwa kwa umakini, na wakachaguliwa

waigizaji wanaovaa uhusika na uhusika ukawavaa wao.


Pamoja na ukweli huo wachambuzi wanasema kwamba kama miaka iliyopita bado tamthilia ni za Udaresalaam, zikidumazwa na misemo na vitabia, lakini haziibui hisia. Watu wanaweza kucheka, wakajitambua lakini hazifikirishi.


Kuna haja ya tamthilia hizi kufuata vigezo vya kitaaluma. Bado, kama ambavyo Bongo Movie zilidumaa zikashindwa kutoboa nje ya nchi kwa kutofikia viwango vya ubora kitaaluma na kimataifa, na tamthilia zetu zitadumaa hivyo hivyo kwa kutofuata vigezo vya

kitaaluma.


“Tuna waigizaji wa kutolea mfano na karibuni tutaona wakitoboa kimataifa, lakini hadithi

zetu bado hazina mvuto wa kuvuka mipaka ya utamaduni wetu ukawagusa wengineo kama

ambavyo Waturuki, Wakorea, Wachina na Wahindi wameweza kutugusa,” anasema.


Katika tuzo hizo Mwigizaji bora wa kiume ilichukuliwa na Hakeem Juma kupitia filamu

ya Dhohari na Mwigizaji bora wa kike ilitwaliwa na Angela Mazanda kupitia Lolita.


Chaguo la wananchi la mwigizaji bora wa kiume ni Romeo Jones kupitia DJ Romy Jones na mwigizaji bora wa kike chaguo la wananchi alikuwa ni Jennifer Kyaka kupitia Fungu Langu.


Pamoja na kila kipengele kushiba katika uchaguzi wa washindi filamu bora mwaka

huu chaguo la wananchi kwenye filamu lilikuwa My Woman huku filamu bora fupi ya Kiswahili ikienda Kenya kupitia sinema ya Kanairo na filamu ndefu ya Afrika Mashariki ilibaki Tanzania kupitia filamu yake ya Sozi.


Ni mafanikio makubwa katika tasnia ya filamu, tuzo hizi zinapomaliza msimu wa tatu.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE