Simulizi : muuaji asakwe...... sehemu ya Nne

 Mtunzi ni: Patrick J. Massawe


Utangulizi


Mwanamke mrembo anauawa ndani ya bafu, nyumbani kwake, eneo la Tabata, Jijini Dar es Salaam. Kwanza kabisa, muuaji huyo katili alimtumia ujumbe wa vitisho muda mfupi tu kabla ya kutekeleza mauaji hayo. Pia, muuaji huyo alimbaka mrembo huyo kabla ya kumuua. Upelelezi wa Jeshi la Polisi, unafanyika mara moja. Msako mkali dhidi ya muuaji huyo unafanyika, na inagundulika siri nzito iliyojificha nyuma ya mapazia kuhusiana na kifo hicho chenye utata. Kama kawaida, mtunzi wako mahiri,  PATRICK J. MASSAWE anatiririka na hadithi hii ya kusisimua.     Fuatilia mpaka mwisho wake…



 “Nzuri…karibu…” John Bosho akajitutumua na kumwambia. Lakini Getruda alinyamaza kimya huku akiiona ile hatari iliyokuwa inamkabili, kwa kusimamiwa na rafiki yake mkubwa, ambaye alionyesha dhahiri alikuwa ana hasira kali!


“Naona wenzangu mnaburudika…”  Anita akaendelea kuwaambia.


“Ah, ndiyo hivyo. Tunapooza makoo baada ya shughuli za kazi…” John Bosho  akasema huku akijiumauma!


“Getruda,” Anita akasema huku akimgeukia.


“Bee…” Getruda akaitikia huku aiangalia chini.


“Naona umeamua kustarehe na shemeji yako…”


“Ndiyo shoga’ngu…tumekutana tu…”


“Si kweli…” Anita akasema na kuonyesha kutomwamini Getruda.


“Huo ndiyo ukweli…nimekutana naye tu, ndiyo maana nikamkaribisha, na mimi sioni ubaya wowote!” John Bosho akadakia!


“Ukweli sasa umejulikana!” Anita akasema na kuongeza. “Nilikuwa nakueleza John, kuwa una uhusiano na shoga’ngu, lakini ukanibishia. Sasa nimewakuta!”


“Yaani kutukuta tumekaa wote ndiyo useme kuwa tuna uhusiano?” John Bosho akamuuliza Anita!


“Ndiyo maana yake…” Anita akamjibu!


“Kwa hivyo?” John akauliza.


“Hakuna cha zaidi, mimi naona kuwa, wewe uendelee na rafiki yangu, Getruda, na mimi niendelee na ustaarabu wangu!” Anita akamwambia kwa hasira John!


“Usifanye hivyo Anita. Mbona unataka kujaza inzi hapa?”


“Ndicho ulichokitaka wewe…”


Wakati wote huo, Getruda alikuwa amenyamaza kimya huku bado akiwa na wasiwasi. Ukweli ni kwamba alikuwa amechanganyikiwa sana, akitamani ardhi ipasuke ajichimbie! Lakini uzuri mmoja ni kwamba Anita akiwa mtu msomi, hakupenda kuzozana mpaka kila mteja aliyekuwa mle ndani ya baa ile ajue kuwa walikuwa wanagombana.


Hivyo basi, Anita aliongea kwa upole huku pia roho ikimuuma sana, na baada ya kumaliza kuwapasha, akauchukua mkoba wake na kuondoka huku akiwaacha John na Getruda wakiwa wanashangaa!


Ukweli ni kwamba lilikuwa fumanizi la nguvu!


“Unaona sasa?” Getruda akamuuliza John!


“Nimeona nini?” John Bosho akamuuliza!


“Si mchumba’ko Anita katukuta? Sijui nani kamwambia tuko hapa?” Getruda akaendelea kusema huku akiwa na wasiwasi mwingi sana!


“Si bure,” John Bosho akasema na kuongeza. “Inawezekana kuna mtu anafuatilia nyendo zetu!”


“Basi, nimetosheka. Sina hamu na kinywaji, mimi naondoka kwenda nyumbani…” Getruda akamwambia John.


“Sawa, tuondoke,” John akasema huku wote wakijiandaa kutoka.


John Bosho na Getruda wakanyanyuka huku wakiacha baadhi ya vinywaji vyao juu ya meza, ambavyo vilikuwa havijamalizika. Kwa mwendo wa taratibu wakatoka hadi nje ya Max Bar, mita chache tu kutoka katika Barabara ya Uhuru iliyokuwa inakatiza mbele ya baa hiyo maarufu.Wakati huo ikiwa imetimu saa moja za usiku, hivyo wakaelekea sehemu ya maegesho alipokuwa amepaki gari lake, ambapo walipanda na kulitoka eneo lile.


John Bosho alimpitisha Getruda nyumbani kwake, Ilala, mtaa wa Moshi, na kumwacha akiingia ndani, halafu yeye akaondoka huku nafsi yake ikimsuta kwa kitendo kile cha kukutwa akiwa na Getruda. Kwani ule ulikuwa siyo uaminifu angali akijua alikuwa na mchumba wake, Anita, waliokuwa wakitarajia kufanya utarataibu wa maandalizi ya kufunga ndoa.


Ni usaliti!


Hata hivyo, baada ya John Bosho kumfikisha Getruda nyumbani kwake, alipanga kwenda Tabata Mawenzi, nyumbani kwa Anita, usiku ule ule ili akamwombe radhi kwa kitendo kile alichokuwa amemfanyia. Ndiyo, alijiamini kuwa angemwagia maneno matamu ya kimapenzi ambayo yangemlainisha na kumfanya asahau masahibu yaliyomkuta!


********          


ANITA alikodi teksi punde tu baada ya alipotoka ndani ya Max Bar. Hakupenda kukaa muda mrefu katika eneo hilo kwa jinsi alivyokuwa amechukia, na alijua kuwa inawezekana John akamfuata nyuma na kuanza kumbembeleza kama ilivyo kawaida yake, ndiyo maana akapenda aondoke eneo hilo haraka sana.


Teksi iliondoka hapo Ilala, na kuifuata Barabara ya Uhuru, ambayo kwa muda huo ilikuwa na foleni kubwa ya magari. Anita alikuwa amekaa kwenye kiti cha nyuma huku amejiegemeza kama mtu anayelala. Hakika hakuamini kile alichokiona kwa macho yake, na hata teksi ilivyokuwa inaendelea na safari kuelekea Tabata, hakuwa na habari kabisa zaidi ya kuzama katika mawazo mazito.


Teksi ilimfikisha nyumbani kwake, Tabata Mawenzi, bila yeye kufahamu kutokana na kuwa na mawazo mengi sana. Ni dereva aliyekuwa anaendesha ndiye aliyemshtua na kumuuliza kuwa anashukia wapi. Ndipo aliposhuka na kulipa fedha, kisha nusu iliyobaki akatembea kwa miguuu kwa kuufuata uchochoro unaolekea nyumbani kwake, ambao unapitia nyuma ya Mawenzi Bar.


Baada ya kufika katika eneo la nyuma yao, akaingia ndani kwa kupitia katika mlango mdogo ulioko katika geti dogo lililotokeza uani. Kisha akaiendea nyumba yake iliyokuwa kule uani, ambayo ni kati ya nyumba zilizojengwa kwa kila mpangaji kujitegemea, inayofahamika kama ‘appatment,’ na kuzungushiwa uzio uliokuwa na urembo wa matundu yanayowezesha kuona upande wa nje.


Nyumba yake aliyopanga, ilikuwa imejengwa kifamilia, ikiwa na vyumba vitatu, sebule, stoo, jiko na huduma ya choo ikiwa mlemle ndani. Mlango mkubwa wa kuingilia ulikuwa upande wa nje kutazamana na uwanja mdogo uliokuwa na bustani nzuri ya maua na miti iliyofungamana na kufanya kuwe na kivuli kizuri wakati wa mchana. Pia, eneo zima lilikuwa limezungukwa na huo ukuta madhubuti.


Anita akatoa ufunguo ndani ya mkoba na kuufungua mlango ule mkubwa. Akaingia ndani na kupokewa na ukimya wa aina yake ukizingatia alikuwa anaishi peke yake. Baada ya kuingia ndani, akawasha taa, halafu akafikia kukaa kwenye sofa lililokuwa pale sebuleni na mkoba wake akauweka juu ya meza. Akabaki akitafakari juu ya kumkuta Getruda na mchumba wake John Bosho wakiwa wamekaa pamoja.


Hata hivyo baada ya kukaa kwa muda, Anita alinyanyuka na kuingia chumbani kwake ili kubadili nguo na kuendelea na ratiba nyingine ya usiku ule.  Alipomaliza kubadili na kuvalia upande wa kitenge, akaingia bafuni na kuoga. Alipomaliza kuoga akarudi tena sebuleni ambako alifungua friji na kuchukua soda moja aina ya Mirinda na kukaa tena kwenye sofa.


Anita aliendelea kunywa soda taratibu, kwani hakuwa na hamu ya kula chakula kabisa, au tusema aliamua kutokula chochote kwa siku ile. Alichokuwa anawaza ni kuachana na mchumba wake, John Bosho mara moja, na pia kuvunja urafiki wake na rafiki yake, Getruda, ambaye kwa muda ule alimfananisha na msaliti aliyeingilia penzi lake.


Ili aweze kuyapunguza mawazo yale, Anita aliwasha runinga na kuendelea kuangalia vipindi vilivyokuwa vinaendelea ingawa ni kwamba alikuwa haelewi chochote zaidi ya kuona kama ni kivuli tu kilichokuwa mbele yake. Mawazo yalikuwa yamemzidi kupita kiasi, hata hivyo, hakupenda mawazo hayo yamwandame zaidi, isipokuwa alichukua simu yake na kuamua kumpigia simu rafiki yake, Getruda, ili amweleze ukweli juu ya kile kitendo alichokuwa amemfanyia!


        ********


UPANDE wa pili. Getruda alibaki hana raha kabisa baada ya kukutwa na rafiki yake, Anita, akiwa na mchumba wake, John Bosho. Ukweli ni kwamba aliweza kuiona hatari iliyokuwa inamkabili, akiwaza kuwa ni lazima Anita angemfanyia kitu kibaya ingawa alikuwa ni rafiki yake wa damu, kutokana na kitendo kile alichofanya.


Getruda alishindwa kabisa hata kumpigia simu rafiki yake, Anita, angalau hata amwombe radhi kwa kile kilichotokea baada ya kumkuta amekaa na mchumba wake, John Bosho. Je, hata angempigia simu, angemwambia nini wakati alikuwa ameshakasirika?”


Wakati Getruda akiwa katika mawazo yale, simu yake ya mkononi iliita. Akaichukua na kuangalia namba za mpigaji, ambayo ilionyesha ni za shoga yake, Anita! Kwanza kabisa kabla hajaipokea simu ile, mapigo ya moyo wake yakaongezeka huku bado akiiangalia ile simu ilivyokuwa inaita.


“Haloo…Anita…” Getruda akaipokea.


“Natumaini hujambo Getruda…” upande wa pili wa simu ukasema.


“Mimi sijambo…”


“Umefurahi sana kunichukulia mchumba wangu sivyo?”


“Hapana Anita…usiseme hivyo!”


“Unabisha?”


“Sibishi…isipokuwa…”


“Sikiliza…” Anita akamwambia na kuendelea. “Sina muda wa kulumbana na wewe! Ukweli ni kwamba umenikwaza sana, na kuanzia leo hii, mimi na wewe urafiki basi, kila mtu aendelee kivyake. Na pia huyo John nakuachia uendelee naye! Nawapa Uhuru!”


“Usifanye hivyo Anita, hayo ni mambo ambayo yanaweza kuzungumzwa. Tambua kuwa tumetoka mbali sana!”


“Kama ulikuwa unatambua kuwa tumetoka mbali, usingenifanyia hayo. Hivyo mimi sina mjadala na kwa heri!” Anita akamaliza kusema!


Akakata simu!


“Mungu wangu!” upande wa pili Getruda akasema na kubaki ameshika simu yake mkononi!


Getruda alikuwa ameshaupata ujumbe ule kutoka kwa rafik yake, Anita. Hivyo hakuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na uamuzi ule, ingawa kwa masikitiko makubwa!


        ********


ALIPOMALIZA kuongea kwa simu na rafiki yake, Getruda, Anita alijibwaga tena kwenye sofa. Wakati akiwa bado amekaa hapo, mara mlango wa nje uligongwa mara mbili. Akashtuka na kubaki akiuangalia huo mlango mkubwa kana kwamba ndiyo kwanza alikuwa ameuona! Mapigo ya moyo wake yakapiga kwa kasi, Je, ni nani anayegonga usiku huo? Hakujua!


Kabla hajanyanyuka kwenda kuufungua huo mlango, mara ukafunguliwa na John Bosho, ambaye aliingia hadi ndani hapo sebuleni, ambapo Anita akiwa bado amekaa, alibaki akimwangalia tu bila kumsemesha, hadi alipoenda kujikalia kwenye sofa dogo la pembeni. Hakutaka kumsemesha Anita ambaye alionekana kuchukia sana, ukizingatia siyo muda mrefu alikuwa akinywa soda yake taratibu tu, kana kwamba hakumwona alivyokuwa akiingia.


“Anita mpenzi wangu…” John Bosho akaamua kumwita baada ya kuvumilia kunyamaza kwa muda.


“Bee,” Anita akaitikia huku akimwangalia kwa huzuni.


“Naona umechukia sana…” John akamwambia kwa sauti ndogo.


“Ni kweli…nimechukia sana!” Anita akamwambia na kuendelea. “Na hata ninapokuona hapa, ni kwamba naona kichefuchefu!”


“Unaona kichefuchefu?” John Bosho akamuuliza!


“Ndiyo, naona kichefichefu! Huwezi kunichanganya mimi na rafiki yangu, Getruda!”


“Ndiyo maana nimekuja tuyamalize mpenzi wangu…”


“Uyamalize na nani?”


“Si wewe mchumba wangu?”


“Haitawezekana kamwe!” Anita akamwambia na kuendelea. “Yaani kuanzia leo hii mimi na wewe basi! Uchumba wetu uishie hapa hapa! Nakuchukia sana!”


“Kwa nini iwe hivyo?”


“Nimejaribu kukuchunguza kwa muda mrefu sasa, na kugundua kuwa wewe siyo mwaminifu kabisa. Hivyo nilichopanga mimi ni kuuvunja uchumba wetu rasmi, hakuna mjadala!”


“Usifanye hivyo Anita…” John Bosho akawa anambembeleza.


“Ndivyo nilivyoamua, mwanaume wewe, unaweza kuniua kwa ukimwi!”


“Usiseme hivyo, ukimwi tena?”


“Ndiyo, huoni unavyoutembeza? Huridhiki na mimi mchumba wako?” Anita akaendelea kusema na kuendelea. “Na kwa taarifa yako, na hii pete ya uchumba uliyonivisha naivua hii hapa!”


“Usiivue tafadhali!” John Bosho akaendelea kumsihi.


“Sikuelewi kabisa!” Anita akasema huku akiivua hiyo pete iliyotengenezwa kwa dhahabu!


John Bosho akabaki akitumbua macho! Baada ya kumaliza kuivua, akampa  pete hiyo ya uchumba kwa kumpatia mkononi mwake, na Jophn akabaki amechanganyikiwa na kuiangalia, kwani hakuamini hicho alichokuwa anakiona! Yaani kurudishiwa pete yake, ambayo alikuwa ameshamvalisha?


“Halafu hatua itakayofuata…” Anita akaendelea kumhabarisha. “Ni kuirudisha nyumba hii uliyopangishia kwa mwenyewe, na mimi narudi nyumbani kwa wazazi wangu, kule Kiwalani, ili niweze kukuachia uhuru wa kutanua vizuri na Getruda! Nimeamua hivyo na hakuna wa kuyabadili mawazo yangu!”


“Unasema unarudi nyumbani kwa wazazi wako?” John Bosho akamuuliza kana kwamba alikuwa hajamsikia vizuri!


“Sina jinsi John. Ukweli ni kwamba nilikupenda sana,” Anita akamwambia na kuendelea. “Lakini sina budi kufanya hivyo!”


“Sijakupata vizuri Anita, ina maana na hii nyumba niliyokupangishia?”


“Hakuna jinsi John, itabidi tuirudishe kwa mwenyewe!”


“Oh,”  John Bosho akaishia kuguna huku akiendelea kumwangalia mchumba wake huyo alivyokuwa amechukua kupita maelezo.


“Halafu kitu kingine ambacho nitakifanya John,” Anita akaendelea kumwambia. “Itabidi nitoe siri zako zote, ambazo nilikuwa nimezificha muda mrefu sasa, kuwa wewe ni mtu mwovu, ni jambazi!”


“Mh! Umefika mbali sasa Anita!” John Bosho akamwambia huku akimwangalia kwa hamaki!


“hapana, sijafika mbali!”


“Ina maana unataka kunichoma?” John Bosho akasema huku akiyatoa macho yake pima!


“Ndiyo, nitafanya hivyo! Na kuanzia sasa hivi ondoka hapa nyumbani!” Anita akamwambia huku akiwa  amechachamaa na povu likimtoka mdomoni!


“Yaani unanifukuza Anita? Hakika siamini!”


“Ndiyo, kuanzia sasa amini! Sitaki mawasiliano na wewe!”


“Hutaki mawasiliano na mimi sivyo?”


“Ndiyo, sitaki!”


“Basi, na mimi nakushauri kuwa fikiria mara mbili mbili juu ya kauli yako ya kutaka kunichoma kwa Jeshi la Polisi! Achana na wazo hilo kabisa!” John Bosho akamwambia Getruda huku akinyanyuka!


“Kwani utafanya nini?”


“Nitajua cha kufanya, naona unajiamini sana wakati unatambua fika kuwa mimi ni mtu wa aina gani!”


“Kabla hujanidhuru, utakuwa umeshatiwa mbaroni!”


“Haya, tuone nani mtoto wa mjini! Mimi naondoka zangu!” John Bosho akamwambia Anita!


Baada ya mabishano yale, John Bosho akaamua kuondoka, kwani hakutaka kubishana na Anita, kitu ambacho kingejaza watu usiku ule. Lakini baada ya kuondoka, alibaki akiwa amechanganyikiwa baada ya Anita kumwambia kuwa angemchoma kwa Jeshi la Polisi, kuwa anajihusisha na ujambazi!


Jambo hilo ndilo lililomuuma zaidi John Bosho! Aliona kama Anita angetoa siri zake, basi huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa kuangamia kwake! Hivyo akaamua jambo moja tu, ni kumwondoa uhai wake haraka iwezekanavyo!


*********          


WIKI moja ilipita tokea John Bosho na Anita kutibuana, mara baada ya kugundulika kuwa yeye ana uhusiano wa kimapenzi na Getruda, rafiki yake Anita. Ukweli ni kwamba wiki hiyo ilikuwa ngumu sana kwa wapenzi wale waliokuwa wameshazoeana. Kila mmoja hakuamini kile kilichokuwa kimetokea zaidi ya kuuamia rohoni.


John Bosho aliendela kumwomba msamaha na kumbembeleza sana, mchumba wake, Anita, lakini hakuambulia kitu zaidi ya kupewa maneno ya kashfa. Kwa vile alikuwa bado anampenda, roho ilikuwa inamuuma sana, hivyo akaamua kukutana na vijana wake wa kazi ili kupanga mkakati maalum.


Walikuwa ni vijana waliokuwa wanajulikana kwa majina ya, Chogolo, Muba, Kessy na Chikwala, ili awaelezee juu ya azma yake ya kutaka kumwondoa uhai Anita, aliyetishia kuitoa siri zake. Kwa kumsikiliza bosi wao, vijana hao wakakubaliana naye na kuzidi kumpa moyo! Ni kumtoa uhai wake mara moja!


Sasa kilichobaki kwa John Bosho, ilikuwa ni juu ya kupanga kifo cha Anita kitakavyotekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu. Kwa upande wake hakupenda kutumia silaha yake katika kutimiza lengo lake, isipokuwa aliamua kutumia sumu kali aina ya nyongo ya Mamba, ambayo huua mara moja mara baada ya mlengwa kuitumia.


Sumu hiyo kali, John Bosho alikuwa anaihifadhi nyumbani kwake kwa malengo maalum, ikiwa katika hali ya unga, lakini akitaka kuitumia, huichanganya na maji tayari kwa kudunga sindano, au unga huo  kwa kuunyunyizia sehemu husika anayokusudia, kama vile kwenye vyakula, maji ya kunywa, vinywaji nk. Hivyo, John Bosho aliamua kummaliza Anita kwa kumdunga sindano ya sumu ile itakayotiwa ndani ya bomba la sindano.


Basi siku hiyo ya kutekeleza kazi yake, John aliiandaa sumu hiyo na kuichanganya na maji, halafu akaiweka kwenye kichupa kidogo, ambacho alikihifadhi ndani ya droo ya gari lake. Baada ya kukamilisha kila kitu, akatoka nje ya nyumba yake, eneo hilo la Ukonga, halafu akapanda gari lake aina ya Toyota Harrier, kuelekea kwenye mizunguko yake mingine ya kibiashara katikati ya jiji la Dare s Salaam.


Alipomaliza mizunguko yake hiyo, ndipo aliposhika uelekea wa kwenda eneo hilo la Tabata Mawenzi, alipokuwa anaishi Anita, mchumba wake waliohitilafiana. Wakati huo ilikuwa imetimu saa saba na nusu za mchana, na yeye alijua kwamba  Anita alikuwepo nyumbani. Hivyo aliifiata Barabara ya Mandela moja kwa moja kutokea Biguruni. Na alipfika eneo la Tabata, alipinda kulia na kuifuata barabara inayoelekea maeneo ya Tabata Bima na kwingineko.


Aliifuata barabara hiyo kwa mwendo wa taratibu tu na baada ya kufika eneo la Tabata Aroma, John Bosho alilisimamisha gari kando ya barabara karibu na kituo cha daladala, halafu akashuka garini na kuelekea kwenye duka moja la kuuza dawa za binadamu, lililokuwa katika jengo lile Aroma, lenye ghorofa tatu.


John Bosho akaingia ndani ya duka hilo kwa kuusukuma mlango wa kioo uliokuwa na fremu ya aluminiam, na baada ya kuingia ndani, alipokewa na hewa ya ubaridi wa kiyoyozi. Humo ndani  alimkuta mwanadada mmoja mwenye umri wakati, aliyekuwa anauza dawa, ambaye alimkaribisha kwa sauti ya kibiashara:


“Karibu…”


“Ahsante…” John Bosho akasema huku akimkagua!


“Nikusaidie…” mwanadada yule akamwambia.


“Ninahitaji bomba la sindano?”  John akamwambia.


“Unahitaji mangapi?…” mwanadada yule akamuuliza.


“Nahitaji bomba moja la sindano…”


“Bomba moja tu?” Muuzaji akauliza baada ya kumshangaa kwa kuchukua bomba moja tu, kwani alitakiwa achukue zaidi ya moja.


“Ndiyo, moja linatosha, kwani vipi?”tu…” John akamwambia huku akimwangalia mara mbili mbili!


 “Naona ungechukua na akiba…moja halitoshi…”


“Kwani unajua nataka kufanyia kazi gani?”


“Si kwa kuchomea dawa?”


“Basi moja linatosha…”


“Haya…” muuzaji huyo akamwambia.


Muuzaji wa dawa akafungua kabati lililokuwa linatunzia dawa, halafu akachukua lile bomba la sidano na kumwekea kwenye bahasha ya rangi nyeupe kwa ajili ya kuwapa wateja. John Bosho akalipokea na kumlipa fedha baada ya kuchomoa noti ya shilingi efu kumi kwenye pochi yake, na kabla hajarudishiwa chenji yake, akaanza kuondoka kuonyesha alikuwa na haraka sana!


John Bosho alifanya hivyo, kwani hakutaka kuulizwa maswali mengi na yule muuzaji, na pia aliogopa sije akamkariri sura itakapogundulika kama ni yeye atakayekuwa ametekeleza mauaji ya Anita, ambapo ndipo alipokuwa anaelekea huko!


“Kaka chenji yako!” Muuzaji yule akamwambia baada ya kuona amesahau!


“Ah, hiyo chenji chukua tu,” John akamwambia, halafu akatoka nje kwa hatua za haraka.


“Ahsante,” muuzaji akasema huku akishangaa kuachiwa fedha na mteja yule!


John Bosho alipofika nje sehemu ile alikopaki gari lake, akaufungua mlango na kuingia ndani. Kabla ya kuondoa gari, akakaa kwa muda, ambapo alifungua droo moja iliyokuwa hapo mbele kwenye ndashibodi ya gari, halafu akatoa kichupa kidogo, ambacho  kilichokuwa na ule mchanganyiko wa maji na sumu kali ya nyongo ya Mamba. Akakakiangalia kichupa hicho huku akitabasamu, hasa akifikiria kuwa ndiyo alikuwa anakwenda kuitumia kwa mlengwa aliyemkusudia!


Mara baada ya kukiangalia kile kichupa kwa muda, akalitoa lile bomba la sindano ndani ya bahasha, na kuinyonya ile sumu kiasi cha kulijaza lile bomba lote, kisha akalirudisha ndani ya bahasha tena na kichupa kukirudisha ndani ya droo. Hapo ndipo alipovuta pumzi ya nguvu na kuishusha, halafu akayatupa macho yake pande zote, kulia na kushoto. Hakuna mtu yeyote kati ya wapiti njia aliyemuoa zaidi ya kila mmoja akiwa katika shughuli zake.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE