"#Save Sudan"... Kampeni kuu kwenye mitandao ya kijamii ikiangazia yanayojiri nchini humo

 Wanaharakati wa mitandao ya kijamii wameanzisha kampeni kubwa iliyopewa jina la Save Sudan inayoangazia na kumulika masaibu yanayowapata wananchi wa Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo na kupuuzwa na jamii ya kimataifa hasa vyombo vya habari ambavyo aghlabu vimeelekeza mazingatio yao huko Gaza na mauaji ya raia wa Palesrina yanayofanywa na Israel.



Hashtagi za #Save Sudan, #talkaboutsudan, na #KeepEyeOnSudan ni sehemu ya kampeni hiyo kubwa iliyozinduliwa na wanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini Sudan ili kumulika ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) dhidi ya raia, haswa baada ya kuingia wapiganaji hao huko Wad Madani, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan.


Kupitia kampeni hiyo, wanaharakati wa Sudan wamechapisha picha za matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa na wapiganaji wa RSF kama vile kuvamia nyumba, kunyakua pesa, kuharibu mali na kuiba kiasi kikubwa cha pesa kutoka benki ya mji wa Wad Madani baada ya jeshi la Sudan kupoteza udhibiti wa mji huo na kuondoka.


Baadhi ya wanaharakati hao wanasema: "Wakati dunia inashughulishwa na mauaji ya watu wa Gaza, Vikosi vya Msaada wa Haraka vinafanya ukiukwaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu dhidi ya raia wa Wad Madani kutokana na kimya cha vyombo vya habari juu ya matukio yanayoendelea katika eneo hilo."


Daktari Anas al Badawi wa Sudan ameandika kwenye akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Kunashuhudiwa kuporomoka kikamilifu mfumo wa afya baada ya maafa ya Wad Madani ambayo ilikuwa kimbilio la wagonjwa." Daktari huyo ameongeza kuwa: "Wanamgambo wa RSF wanaharibu vituo vya afya katika miji yote, kupora vifaa vya matibabu, na kuwaua na kuwateka nyara madaktari na wahudumu wa afya."


Baadhi ya wanaharakati wa mitandao ya kijamii wa Sudan wameandika kuwa: "Watu wa Sudan wanakabiliwa na nyakati za kutisha ambazo ni vigumu kufikirika na kueleweka. Watu wanazikwa wakiwa hai magharibi mwa Sudani, nyumba za raia zinaharibiwa na wanawake wanabakwa."


Juhudi za upatanishi wa kuhitimisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan zimeambulia patupu hadi sasa huku kila mmoja kati ya wababe wa vita hivyo, Abdel Fattah Al-Burhan na Jenerali muasi, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), akiendelea kung'ang'ania misimamo yake.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE