Jeshi la Polisi Kikosi Cha Usalama Barabarani limetoa onyo kwa madereva wanaokiuka sheria na kanuni za usalama barabarani na kusema watawatoza faini za papo kwa papo pamoja na kuwafikisha Mahakamani.
Onyo hilo limetolewa hii leo Desemba 24, 2023 na Afisa Mnadhimu Makao makuu ya Trafiki nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Pili Misungwi wakati akizungumza na Madereva, Abiria na Mawakala wa mabasi stendi kuu Makatanini iliyopo Babati Manyara.
Amesema, madereva, abiria na mawakala hao wanatakiwa kuzingatia sheria kwa kujali matumizi sahihi ya barabara na kuepuka kupakia abiria kupita kiasi kwani imekatazwa kisheria.
Aidha, amewatahadharisha madereva kukagua vyombo vyao vya moto mara Kwa mara kabla ya kuanza safari ili kubaini kama kuna changamoto iweze kutatuliwa mapema kabla haijasababisha ajali.
Awali, Kamanda wa Kikosi hicho Mkoa wa Manyara Mrakibu wa Polisi, Fredinand Mpolo amemuhakikishia Kamishna huyo kuwa watafanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha wanawakamata madereva wazembe barabarani.
Kamishna Misungwi yupo Mkoani Manyara katika ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi wa Askari kikosi hicho, pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na abiria.
0 Comments