Mwanafunzi atoweka katika mazingira ya kutatanisha Moshi

 

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Bendel, iliyopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Vaileth Makundi (13) ametoweka baada ya kutoonekana nyumbani kwao kwa siku nne, huku akiacha ujumbe wa maandishi.


Vaileth ambaye alikuwa akisoma shule hiyo ya bweni, alitoweka nyumbani kwao tangu Desemba 6, mwaka huu siku moja baada ya kuchukuliwa shuleni kwao na bibi yake aliyekuwa akiishi naye baada ya shule kufungwa Desemba 5.


Akizungumza nasi jana Desemba 9, bibi wa mwanafunzi huyo, Clara Maleko amesema mjukuu wake huyo alitoweka nyumbani kwao siku ya Jumatano, Desemba 6 na kuacha ujumbe wa maandishi akiandika, "bye bye wote."


Bibi yake huyo, amesema baada ya  mwanafunzi huyo kutoweka nyumbani kwao siku hiyo,  alikwenda kituo cha Polisi cha Himo kutoa taarifa za kutoonekana kwa mjukuu wake huyo ambapo alipewa RB namba Him/RB/3724/2023 na mpaka sasa hajaonekana.


"Nilipigiwa simu siku ya Desemba 5, kwenda kumchukua mjukuu wangu shuleni, kwani walikuwa wanafunga shule siku hiyo, nilifika shuleni na kumchukua na kurudi naye nyumbani muda wa saa kumi jioni.


"Nilipofika naye nyumbani tulipika chakula cha jioni tukala pamoja, tulilala mpaka asubuhi ya Desemba 6 kulipokucha, siku hiyo tulipoamka yeye alikuwa ndani anafanya usafi na mimi nikawa nje naosha vyombo, ilichukua muda mrefu sana kama saa mbili hivi hajatoka ndani na wakati huo nilikuwa niko nje bado," amesema.


Amesema baada ya kukaa muda mrefu bila kumwona aliingia ndani na kumuita akidhani yuko chumbani na hakuitika, aliingia vyumba vyote kumuangalia hakumwona na aliporudi sebuleni alikuta mlango wa mbele umefunguliwa, alitoka tena nje kumwangalia hakumuona.



"Nilirudi tena chumbani kwangu kumwangalia, nikakuta kikatarasi kitandani kimeandikwa “bye bye wote,” nilipiga simu kwa baba yake na mama yake na maeneo mengine kama wamemwona wakanambia hawajamuona, ndipo nilipochukua hatua ya kwenda polisi kutoa taarifa.”


Ameeleza kuwa ameshazunguka maeneo mengi kumuulizia mtoto huyo bila mafanikio, akiomba serikali na jamii imsaidie.


"Tangu Desemba 6 mjukuu wangu apotee katika mazingira ambayo sijayaelewa nimeshindwa hata kula, silali, nimeishiwa nguvu na leo ni siku ya nne sijapata kabisa usingizi maana sijui kama mjukuu wangu yupo hai au lah," amesema.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuhusiana na tukio hilo simu yake iliita zaidi ya mara nne na haikupokelewa.


Hata hivyo, Mwananchi Digital ilimtafuta Makamu mkuu wa shule hiyo, Assey Pamphilus, ambapo amesema kwa kuwa mwanafunzi huyo amepotea wakati shule zimeshafungwa watafanya jitihada za kuwasiliana na wazazi wa wanafunzi waliokuwa wanasoma na mwanafunzi huyo ili kujua ni nini kimetokea.


"Jumatatu nitaenda ofisini ili tujue kuna nini maana niko likizo, tutawatafuta wazazi wa wanafunzi ambao walikuwa marafiki na mwanafunzi huyu, tutamtafuta mmoja baada ya mwingine kupitia walimu wetu ili tujue," amesema mwalimu huyo.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE