Mvua ya nusu saa yakosesha makazi watu 300 Kilosa

 Zaidi ya wananchi 300 wamekosa mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kuingiliwa na maji wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 10, 2023.



Mvua hiyo iliyonyesha kwa muda wa nusu saa, pamoja na kusababisha athari kwa makazi ya watu, pia imeathiri madaraja manne yakiwemo madaraja ya muda ya Mazinyungu na Wa Ilonga, yanayounganisha mji wa Kilosa, Dumila na maeneo mengine.


Madhara mengine ni kumeguka kwa sehemu ya maungio ya daraja la Mto Mkondoa, panapoungana reli, daraja na barabara ambazo zimemeguka sehemu kubwa na kufanya barabara ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi na maeneo mengine ya ukanda huo kushindwa kupitika kwa vyombo vya moto.


Hasanaly Kombo, akizungumza na Mwananchi Digital katika eneo la Manzese B wilayani Kilosa, amesema nyumba zimeingiliwa na maji, kubomoka, huku vyakula na mali nyingine kama mavazi vikiondoka na maji.


Maua Shomary, amesema anaamini mafuriko hayo ni makubwa kuwahi kutokea katika maeneo hayo, ingawa anaamini yamesababishwa na tuta la reli ya treni ya kisasa (SGR) inayokatiza eneo hilo.


Pia amesema usumbufu wa maji umekuwa wa mara kwa mara hasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu kujengwa kwa tuta hilo.


Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema wanaendelea na tathmini zaidi kujua athari zilizopatikana, ingawa kwa awali kaya zaidi ya 70 zenye wakazi zaidi ya 300 zimebainika kuathiriwa na mvua.



“Pamoja na athari hii kubwa, pia madaraja zaidi ya manne yako kwenye hali mbaya miongoni yamezolewa kabisa na maji, bado hatuna taarifa zozote za kifo wala majeruhi," amesema Shaka.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Malima amewasihi wananchi wasisogelee maeneo yaliyozolewa na maji, kwani yameacha hatari nyingine ya mmomonyoko wa udongo unaoweza kuleta maafa makubwa zaidi.


Malima amesema licha ya kuendelea na tathmini, bado wananchi wengine wamejitakia kufuatwa na mafuriko kwa waliojenga kwenye mkondo wa maji, hivyo kuwasihi waondoke kupisha maeneo hayo.


Amesema vijiji zaidi ya saba wilayani Kilosa vimeathiriwa na mvua zilizonyesha ndani ya kipindi kifupi.


“Tunajua msaada wa kwanza unaohitajika ni chakula na tunaendelea kuhakikisha mtapata chakula kwa sababu hata akiba ya chakula mlichokuwa nacho ndani kimeondoka au kuharibiwa na maji,” amesema.


Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema watafanya jitihada za haraka kuhakikisha barabara na madaraja yaliyoharibika yanatengenezwa haraka, ili njia zipitike kama kawaida.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE