Mchongo wa ajira 500 za uuguzi Saudi Arabia watangazwa

 Dar es Salaam. Serikali imetangaza fursa ya nafasi 500 za  ajira za wauguzi wa kike kuajiriwa na Serikali ya Saudi Arabia Januari 2024.



Utangazwaji wa ajira hizo ni wazi  unafuta ile dhana iliyojengeka kuwa  Watanzania hawapati ajira nje ya nchi ikilinganishwa na mataifa mengine Afrika yanayopigiwa  mfano katika eneo hilo kuwa na  idadi kubwa ya vijana wanaoajiriwa ughaibuni.


Taarifa hiyo imetangazwa Dar es Salaam leo Jumatatu Desemba 8, 2023 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhandisi Cyprian Luhemeja, huku akisema sifa awe Mtanzania mwenye elimu ya kuanzia diploma na  mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 31 mwaka huu.



"Tumepata fursa za ajira kwa Watanzania wenzetu wa kike 500  kwenda kufanya kazi Saudi Arabia.  Tunaomba Watanzania wote wenye sifa na ujuzi uliobainishwa waombe kazi husika kwa kujisajili https://jobs.kazi.go.tz na kutuma wasifu binafsi (CV)," amesema


Amewaomba Watanzania kuchangamkia fursa hiyo haraka kwani mchakato wake wa kuwapata unapaswa kukamilika kufikia Januari 10 mwakani.


"Kwa watakaofanikiwa watakutana na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako Januari 10, 2024, kwa hiyo tuna muda mfupi na hatutumii makaratasi bali ni mitandao," amesema.


Amesema baada ya mazungumzo na Waziri Ndalichako, Watanzania hao watafanyiwa mchakato wa kuongea na Serikali ya Saudi Arabia kisha kuwafanyia mipango ya usafiri kwenda kuanza kufanya kazi.


Amesema mafanikio hayo ni jitihada zilizofanywa na Serikali katika kuingia hati za makubaliano inayohusiana na  ajira na  Serikali ya Saudi Arabia na  Umoja wa Falme za Kiarabu.


"Lakini pia Serikali bado inakamilisha mazungumzo yanayoendelea kati yetu  na nchi 10 ikiwemo Australia tunayotarajia kusaini nayo mkataba kuanzia Januari mwaka 2024  ili kuendelea kutoa fursa kwa watanzania kwenda nje ya nchi," amesema


Katika kutimiza azma hiyo kwa ufanisi Mhandisi Luhemeja ametoa rai kwa Watanzania wote wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo katika fani zote wenye nia ya kufanya kazi nje ya nchi, kujisajili Kitengo cha Huduama za Ajira (TaESA).

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE