KIGOMA: CHAMA cha, ACT Wazalendo leo kimezindua mchakato wa uchaguzi wa ndani kwa ajili ya kuwapata viongozi wake wa ngazi ya mkoa ambapo mkoani Kigoma Waziri Kivuli wa Mifugo na Uvuvi wa chama hicho, Kiza Mayeye amejitokeza kuchukua fomu kwa ngazi ya nafasi ya uenyekiti wa ACT mkoa Kigoma.
Mchakato huo umezinduliwa rasmi na Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma, Juma Ramadhani ambaye amesema kuwa uchukuzi wa fomu kwa ngazi mbalimbali za uongozi mkoani humo zimeanza kutolewa Desemba 28 hadi Januari 9 mwakani zoezi litakapofungwa kusubiri uchaguzi utakaofanyika Januari 12 mwakani.
Ramadhani ambaye ni Mwenyekiti wa uchaguzi wa chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma amesema kuwa kwa nafasi ya Mwenyekiti wa mkoa na ngome za vijana, wazee na wanawake fomu zitatolewa kwa kiasi cha shilingi 10,000 ambazo zitalipwa benki kwa kupitia akaunti ya chama hicho mkoani Kigoma.
Katika uzinduzi huo wa uchukuaji fomu Waziri Kivuli wa mifugo na uvuvi ACT wazalendo, Kiza Mayeye amejitokeza kuchukua fomu kwa nafasi ya uenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Kigoma ambapo Mwenyekiti wa chama hicho jimbo la Kasulu, Haruna Kwasakwasa alichukua fomu hiyo kwa niaba yake.
0 Comments