Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeanza kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu uliogubikwa na machafuko huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wakidai kuwa kumekuwa na dosari nyingi katika mchakazo mzima wa upigaji kura.
Tume ya uchaguzi, CENI, siku ya Ijumaa ilitangaza matokeo ya upigaji kura wa Wakongo wanaoishi Afrika Kusini, Marekani, Kanada, Ubelgiji na Ufaransa huku matokeo ya ndani ya nchi yakitazamiwa kuanza kutangazwa baadaye leo Jumamosi.
Kura hizo, ambazo zinawakilisha sehemu ndogo ya wapiga kura, zimeonyesha Rais Felix Tshisekedi akiwa mbele sana ya wapinzani wake. Wapigakura pia walipiga kura kuwachagua wabunge wa kitaifa na wa mikoa, na madiwani wa serikali za mitaa.
Matokeo hayo ya muda yanakuja baada ya upigaji kura katika taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini la Afrika ya Kati kuongezwa hadi Alhamisi baada ya baadhi ya vituo kushindwa kufunguliwa kwa umma na baadhi ya wapiga kura kukosa majina yao kwenye daftari la wapiga kura.
Kuongezwa muda wa kupiga kura kulizua mvutano mkali kutoka kwa wagombea wa upinzani, ambao baadhi yao walitaja hatua hiyo kuwa ni kinyume cha katiba na hivyo wanataka uchaguzi inaojumuisha mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege na mfanyabiashara mkubwa na gavana wa zamani Moise Katumbi urudiwe.
Licha ya tume ya uchaguzi kutangaza kuwa vituo vya kupigia kura havijaidhinishwa kufunguliwa zaidi ya Alhamisi, upigaji kura uliendelea katika baadhi ya maeneo, hasa maeneo ya mbali, hadi Ijumaa.
Waangalizi huru wameibua wasiwasi kuhusu kura hiyo. Hata hivyo, Denis Kadima, mkuu wa tume ya uchaguzi nchini humo, siku ya Ijumaa alipuuzilia mbali ukosoaji kwamba kuongeza muda wa kupiga kura kulipelekea zoezi la uchaguzi kukosa itibari ya kisheria.
CENI imeweka Desemba 31 kuwa tarehe ya mwisho ya kutolewa matokeo kamili ya muda, lakini haijulikani kama hilo litabadilika kutokana na kurefushwa muda ambako hakukutarajiwa kuhusu zoezi hilo la upigaji kura.
DRC, ambayo ni mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani licha ya kuwa na akiba kubwa ya shaba, kobalti na dhahabu, ina historia ya chaguzi zinazozozaniwa ambazo zinaweza kugeuka kuwa machafuko makali.
Uchaguzi wa Tshisekedi kama rais mwaka 2018 ulikumbwa na shutuma za wizi wa kura na udanganyifu.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 34 waliuawa na wengine 59 kujeruhiwa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.
0 Comments