Marekani yaikatisha tamaa Ukraine, onyo la Zelensky

 Kuendelea mvutano kati ya Warepublican na Ikulu ya White House juu ya kupasishwa msaada mpya kwa Ukraine, pamoja na kutoa kipaumbele Washington kwa vita vya Gaza na natija yake kusahaulika vita vya Ukraine, kumepelekea serikali ya Biden kuitahadharisha Kyiv kuhusu uwezekano wa kukatiwa au kupunguziwa kiasi kikubwa cha misaada yake.


Matthew Miller Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani alisema Jumanne kwamba: Hatuna bajeti ya kimiujiza ya kusaidia Ukraine. Ikiwa bunge la Congress halitapitisha mswada huu (kifurushi cha kifedha cha Biden), hatutakuwa na pesa za kusaidia Ukraine. Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema: Tumetumia fedha zilizopo na katika kipindi cha wiki chache zijazo hakutakuwa na pesa zilizosalia.


Awali, John Kirby, Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la White House, pia alitangaza uwezekano wa kumalizika bajeti ya Ukraine mwezi huu iwapo bunge halitaidhinisha mswada uliopendekezwa na Rais Joe Biden wa Marekani kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kirby amesisitiza kuwa utawala wa Biden unapanga kutangaza kifurushi kingine cha msaada wa kijeshi kwa Ukraine mwezi huu na kabla ya kumalizika mwaka, lakini baada ya hapo, bajeti ya Ukraine itaisha. Mdhibiti wa Fedha wa Pentagon Mike McCord hivi karibuni aliliandikia barua bunge akilitaka kuchunguza kifurushi cha bajeti ya Biden ya dola bilioni 106. Kwa mujibu wa mswada huo, Ukraine ilikuwa imetengewa dola bilioni 61.7. Aliandika kwenye barua hiyo: Bunge linapaswa kuchukua hatua bila kuchelewa kuhusiana na bajeti ya ziada ya serikali na kufanya hivyo ni kwa maslahi ya taifa letu na ni muhimu kwa uhuru wa Ukraine.


Marekani, ikiwa ni mhimili muhimu wa kijeshi na wa silaha kwa Ukraine, katika miezi kadhaa imekuwa ikikabiliwa na tofauti na mivutano mikubwa bungeni. Mabunge ya Congress ambalo lina wingi wa wabunge wa Republican na Senati ambayo inadhibitiwa na wabunge wa chama cha Democrate, hadi sasa bado hayajapitisha bajeti ya mwisho ya mwaka mpya wa fedha, ulioanza mwezi Oktoba. Serikali ya shirikisho kwa sasa inaendesha shughuli zake kwa nyongeza ya dharura ambayo itaisha katikati ya Januari 2024. Ni kutokana na sababu hiyo ndipo hadi sasa, bunge la nchi hiyo halijapitisha bajeti mpya kwa ajili ya kusaidia Ukraine. Wakati huo huo, Warepublican waliowengi bungeni wamezuia kuidhinishwa bajeti iliyopendekezwa na Ikulu ya Marekani kwa ajili ya Kyiv, na hii ina maana ya kumalizika uungwaji mkono mkubwa  wa vita nchini Ukraine. Warepublican, bila kujali tofauti zao kuhusu vita vya Ukraine, wanataka kupunguza matumizi ya serikali ya shirikisho na wanaamini kuwa serikali ya Biden inapaswa kupunguza bajeti na kuzuia kuongezeka deni la serikali kuu ya shirikisho. Inaonekana kuwa itakuwa vigumu kupitishwa bajeti ya kifedha ya serikali ya Biden, ambayo inajumuisha msaada kwa Ukraine na wajumbe wa Congress, hasa Warepublican, ambao wanatoa kipaumbele kwa suala la usalama wa mipaka ya nchi hiyo. Serikali ya Marekani, ambayo hadi sasa imekuwa ikisimama na Kyiv ili kuishinda Russia katika vita na Ukraine, inasisitiza kuwa iwapo Congress haitapitisha bajeti iliyokusudiwa na Ikulu ya Marekani ndani ya mwezi mmoja ujao, haitaweza kuisaidia Ukraine na bila shaka iwapo msaada wa Washington hautaifikia Ukraine, itashindwa tu katika vita na Russia.


Ukraine inalalamikia kupungua misaada ya Magharibi kwa nchi hiyo na imetoa maonyo kadhaa kuhusiana na suala hilo. Katika msimamo wake  kuhusu suala hilo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema kuwa mzozo wa Mashariki ya Kati umeelekeza fikra za waliowengi duniani upande wa Israel na kutengwa Kyiv katika uwanja huo. Amesema nchi nyingi za Magharibi sasa ziko kwenye shaka na hali ya kusitasita iwapo zitatoa msaada kwa Kyiv au Tel Aviv.  Akiashiria kwamba kudumishwa misaada ya kimataifa kwa Ukraine kunazidi kuwa kugumu kila siku, Zelensky amesisitiza kwamba hali hii itaacha athari mbaya sana kwa Ukraine katika medani ya mapigano. Nchi nyingi za Magharibi sasa zinasitasita ziisaidie Ukraine au Israel. Ukosoaji wa rais mwenye mielekeo ya umagharibi wa Ukraine kuhusu kupunguzwa misaada ya kijeshi na silaha kwa Kyiv katika vita vyake na Russia unaonyesha mkondo mpya wa kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani kutoka Ukraine kuelekea nchi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza. Suala hilo limewapa wasiwasi mkubwa sana watawala wa Ukraine. Licha ya ahadi za kuendelezwa msaada wa silaha kwa Ukraine, serikali ya Biden imetoa kipaumbele kwa suala la kukidhi mahitaji ya kijeshi ya Tel Aviv, na nchi za Ulaya haziko tayari au haziwezi tena kuendelea kutoa msaada wa kijeshi na silaha kwa Kyiv kama ilivyokuwa hapo awali.


 

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE