Mapitio gharama za NHIF yanamaanisha nini?

 Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umefanya mapitio ya kitita cha mafao kwa mwaka 2023, ambayo yanalenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma ili kuendana na bei halisi ya soko.


Moja ya maeneo ambayo marekebisho hayo yanakwenda kuwagusa watumiaji wa huduma ni kupunguza gharama za kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo.


Kwa mujibu wa mfuko huo, maboresho hayo pia yanakwenda kupunguza gharama kwa wanachama waliokuwa wakilazimika kununua baadhi ya dawa ambazo hazikujumuishwa kwenye kitita cha mafao huku dawa 124 zikiongezwa kwenye Orodha ya Dawa Muhimu ya Taifa (NEMLIT).


“Tumekuja na maboresho haya baada ya majadiliano na watoa huduma na wadau mbalimbali, lakini pia tulifanya utafiti wa kina na kujiridhisha, baadhi ya huduma zinazotolewa haziendani na gharama halisi za soko, tumebaini ama zipo juu au chini, hivyo tumefanya marekebisho,” alisema Bernard Konga, mkurugenzi mkuu wa mfuko huo.


Konga alisema hayo jana katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, juu ya maboresho ya Kitika cha Mafao 2023.


Maboresho hayo yamefanyika pia upande wa ada ya kumuona daktari, aliyosema awali ilikuwa inategemea taaluma ya daktari bingwa katika hospitali za rufaa na ya Taifa sambamba na zile za mkoa.


Konga alisema ada hiyo baada ya maboresho, itakuwa sawa kwa lengo la kupunguza msongamano ambao upo hivi sasa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako asilimia kubwa ya madaktari bingwa wanapatikana.


Alisema Serikali imewekeza kiwango kikubwa kwenye sekta ya afya ikiwemo kufunga mashine za CT-Scan kwenye hospitali zote za mikoa, hivyo lazima vifaa hivyo vitumike kusaidia Watanzania.


Yataleta unafuu


Kufuatia mabadiliko hayo, Rais wa Chama cha Madaktari wa Macho Tanzania, Asha Mweke alisema mabadiliko yaliyofanyika yanakwenda kuleta nafuu kwa mlaji ambaye ni mwananchi na matamanio yao ni kuona wananchi wakipata huduma bora za afya.


“Mwananchi sasa ataweza kumuona daktari bingwa na daktari bobezi kwa gharama nafuu na kwa uharaka zaidi badala ya kwenda kulundikana kwenye hospitali moja, tusubiri tutaona nafuu zaidi wakati wa utekelezaji,” alisema.


Mtaalamu mwingine na mshauri wa masuala ya afya ya jamii, Dk Festo Ngadaya alisema mabadiliko hayo yanakuja katika kipindi ambacho Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote imepitishwa, hivyo huenda kwa NHIF ni kama majaribio.


Hata hivyo, alisema malalamiko ya wananchi hayakuwa kwenye gharama za kumuona daktari, bali gharama za vipimo, upasuaji na wagonjwa kulazwa, hivyo hayo ndiyo maeneo yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi.


Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah alisema mabadiliko ya fedha za kumuona daktari, yasitafsiriwe kama ni fedha za daktari.


“Imechukuliwa sehemu nyingine kama fedha hizo ni za daktari, wakati mwingine daktari anachukua, lakini tafsiri ya ada hii ni kwamba, hata wataalamu wengine wa afya wanaomsaidia daktari wanapaswa kupata fedha hizo,” alisema.


“Lakini nionavyo mimi, maboresho haya pia yanalenga kuhamasisha bima kuvutia wagonjwa wanaotaka kupata huduma ya madaktari bingwa, kwa hiyo wigo wa bima unakwenda kuongezeka,” alisema.


Hezekiah alisema kwa sasa mabadiliko hayo ni kutokana na uhalisia wa uendeshaji wa huduma za afya kuwa endelevu kulingana na gharama zilizopo sokoni. Aliongeza kuwa huenda kukawa na changamoto katika utekelezaji wa bei hizo, kama sekta binafsi haikushirikishwa vema, “lakini kama walishirikishwa vema katika kufanya maboresho haya, sioni tatizo.”


Gharama usafishaji figo chini


Akizungumzia huduma ya usafishaji figo, Konga alisema kutokana na maboresho hayo ambayo yanaanza kutumika rasmi Januari mosi 2024, wagonjwa wa figo ambao walikuwa wakisafishwa damu kwa Sh240,000, sasa watatumia Sh200,000.


“Tumegundua gharama haikuwa inaakisi gharama za soko, hivyo tumepunguza,” alisema.


Kwa mujibu wa NHIF, maboresho hayo pia yanaenda kupunguza gharama kwa wanachama waliolazimika kununua baadhi ya dawa, ambazo hazikujumuishwa kwenye mfuko wa mafao.


“Mapitio hayo tuliyofanya yanalenga kuongeza au kupunguza gharama katika baadhi ya huduma ili kuendana na bei za soko,” alisema


"Hakuna haja ya kufanyia kipimo cha CT-Scan kwenye Hospitali ya Taifa wakati huduma hiyo hiyo unaweza kuipata katika hospitali za mkoa, hivyo kupitia maboresho hayo tutaangalia aina ya rufaa ambazo zinatolewa na hii itasaidia kuongeza motisha kwa madaktari," alisema mkurugenzi huyo.


Alisema maboresho pia yataangazia baadhi ya wanachama ambao wanafanya kipimo kimoja kwenye zaidi ya hospitali moja.


"Unakuta mwanachana ametoka hospitali A kupima malaria lakini muda mfupi mgonjwa huyu huyo anakwenda kituo B na C kwa siku moja, hilo ni kosa.


“Na kuna baadhi ya kipimo mfano ECHO, ukipima mara moja majibu ni hayo hayo, hayawezi kuwa tofauti hata kama utaenda kupima sehemu nyingine. Hivyo tumetengeneza jukwaa la kieletroniki litakalowezesha watoa huduma kubadilishana taarifa za mgonjwa baina ya kituo kimoja na kingine,” alisisitiza.


Hata hivyo, Konga alisema maboresho hayo si kwamba ndiyo yameishia hapo, bali NHIF itaendelea kupokea maoni ya wadau kwa lengo la kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma bora kwa wanufaika wote wa mfuko.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE