Kondakta wa Basi la Kampuni ya ABC aliyetambuliwa kwa jina moja la Pendo, amefariki dunia, huku watu 12 wakijeruhiwa baada ya basi hilo kuligonga lori lililokuwa limeegeshwa eneo la Chinangali mkoani hapa.
Majeruhi wa basi hilo wamesema ajali hiyo ilitokea jana saa 4.00 usiku wakiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Dodoma.
Akizungumza leo Jumatano Desemba 13, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, mkazi wa Nkhungu mkoani hapa, Theodata Bali amesema ametokea Zanzibar yeye na mjukuu wake ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne, Baraka Waldi.
Amesema waliondoka saa 7.30 mchana jijini Dar es Salaam na mwendo wa dereva wa basi hilo hakuwa mzuri tangu walipoanza safari.
“Tulinusurika kupata ajali mkoani Morogoro ilikuwa alivae Semi trailer upande wake. Bahati lile semi treiler lilikuwa na breki nzuri kwa hiyo lilifunga breki na yeye (basi) akafunga breki na kuzimika papo hapo,” amesema.
Amesema yeye hupanda mabasi hayo mara nyingi lakini kwa siku ya jana alishangaa mwendo wa basi hilo, lakini waliponusurika kwa mara ya kwanza akajua atajirekebisha.
Hata hivyo, amesema hali ilibadilika kwa muda lakini lilipoanza kuingia giza alianza tena kuongeza mwendo na walipofika Chinangali ndipo walipata ajali, baada ya basi hilo kuligonga lori kwa nyuma. “Nilikuwa nimeanza kusinzia nilipostuka nikakuta mbele ya basi kote kuko wazi. Mimi nilikuwa nimekaa nyuma ya kiti cha kondakta nilirukiwa na vioo, ndio maana macho yamekuwa mekundu, mbele yetu alikuwa amekaa kondakta (aliyefariki), alikuwa amebanwa sana,” amesema.
Amesema alikuwa amebanwa miguu hivyo walivutia kiti ndipo akaitoa. “Dereva wa basi alitimua mbio baada ya kusababisha ajali,”amesema. Amesema yeye amepata jeraha mkononi, uso na machoni kutokana na vioo vilivyomruhia, huku mjukuu wake akijeruhiwa katika kidevu ambapo amefanyiwa upasuaji leo asubuhi.
Majeruhi mwingine ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo aliyekuwa akitokea jijini Dar es Salaam kuchukua mzigo, Eva Kiondo amesema dereva huyo alikuwa katika mwendokasi na walipofika Chinangali alisikia kishindo kikubwa.
Amesema kwa kuwa alikuwa amefunga mkanda, alijigonga uso na kupata majeraha ambayo yalisababisha kuvuja kwa damu nyingi.
“Nilipojiangalia nilijikuta nimejaa damu kwenye gauni zima nililoliva. Walivunja mlango wa nyuma wa basi ambapo ndipo walitutoa abiria mmoja baada ya mwingine. Tukiwa pale bahati nzuri alipita mtoto wa shangazi yangu akanichukua na kunileta hapa,” amesema.
Ofisa Mawasiliano na Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Renatha Mzanje amesema mwili wa kondakta huyo na majeruhi 12 walipokelea saa 5.00 usiku wakitokea kwenye ajali ambayo ilitokea wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Amesema kati ya majeruhi hao tisa walitibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani huku wengine watatu waliokuwa katika hali mbaya wakilazwa hospitalini hapo.
“Marehemu ametambulika kwa jina la Pendo juhudi zinaendelea kupata watu wanaomtambua zaidi ili iwe rahisi kupata ndugu zake. Majeruhi waliolazwa wanaendelea vizuri baada ya kuhudumiwa,” amesema Renatha.
Akizungumza nasi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema yuko katika kikao na atawasiliana na mwandishi baadaye. Hata hivyo, alipotafutwa baadaye kwa zaidi ya mara tano kwa nyakati siku yake iliita bila kupokelewa.
0 Comments