Serikali ya Somalia imetangaza kwamba imemuua Maalim Ayman, kiongozi mwandamizi wa Kundi la Al Shabaab katika oparesheni ya pamoja kati ya jeshi la nchi hiyo na Jeshi la Marekani.
Waziri wa Habari wa Somalia, Daud Aweis, ametangaza kwamba Ayman aliuawa Desemba 17, 2023.
“Ayman alikuwa na jukumu la kupanga mashambulizi ya kigaidi kadhaa yenye madhara nchini Somalia na nchi jirani,” Aweis alisema katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, Ayman alihusika na shambulio la kigaidi dhidi ya raia wa Marekani na Kenya katika Uwanja wa Ndege wa Manda Bay nchini Kenya mnamo Januari 5, 2023.
Raia watatu wa Marekani walipoteza maisha, akiwemo mwanajeshi mmoja na wakandarasi wawili. Maafisa wengine wawili wa Marekani na mkandarasi mmoja walijeruhiwa katika tukio hilo.
Serikali ya Marekani iliweka zawadi ya hadi dola milioni 10 kwa yeyote atakayetoa habari zitakazosaidia kukamatwa au kuhukumiwa mahakamani popote duniani kwa Maalim Ayman Januari, mwaka huu.
Al-Shabaab iliorodheshwa na Marekani kama kundi la kigaidi mwaka 2008 na na kamati ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2010.
0 Comments