Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa sera za kamupini ya Meta zimezidi kuziba na kunyamazisha sauti zinazoiunga mkono Palestina kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook kutokana na vita vya Israel dhidi ya Gaza.
Ripoti ya Human Rights Watch imeeleza kwamba kuna mtindo wa kuondolewa na kufuta bila sababu maudhui zinazoiunga mkono Palestina, ikiwa ni pamoja na maudhui ya kujieleza kwa amani na mjadala wa umma kuhusu haki za binadamu za Wapalestina.
Ripoti hiyo yenye kurasa 51 iliyotolewa jana Alhamisi yenye kichwa cha habari “Kuvunja Ahadi...Sera za Meta na Udhibiti wa Maudhui Yanayohusiana na Palestina kwenye Instagram na Facebook,” imeeleza kuwa tatizo hilo linatokana na kasoro za sera na utekelezaji wa kampuni hiyo ambayo imeathiriwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na "ushawishi usiofaa wa serikali kuhusu ufutaji wa maudhui".
Debra Brown, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Teknolojia na Haki za Kibinadamu katika Human Rights Watch, amesema kuwa udhibiti wa Meta wa maudhui yanayounga mkono Palestina "unafanya mambo kuwa mabaya zaidi kutokana na ukatili wa kutisha na ukandamizaji wa aina mbalimbali ambao tayari unazima na kuzuia sauti za kujieleza za Wapalestina."
Debra Brown ameongeza kuwa: "Mitandao ya kijamii ni majukwaa muhimu ambayo yanaruhusu watu kushuhudia ukiukwaji wa haki za binadamu na kueleza upinzani wao dhidi na mambo hayo, lakini udhibiti wa Meta unazidisha njama za kufichwa mateso ya Wapalestina."
Itakumbukwa kuwa, wiki kadhaa zilizopita wanaharakati kote ulimwenguni walizindua kampeni ya "Hatutanyamazishwa" (wewontbesilenced#) kupinga sera za kampuni ya Meta ya Marekani inayomiliki mitandao kadhaa ya kijamii, ya kuzuia au kufuta maudhui yanayoiunga mkono Palestina, hasa kwenye majukwaa ya "Facebook" na "Instagram".
Kampeni hiyo, ambayo ilizinduliwa sambamba na Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina na bado inaendelea, ilitoa wito kwa wanaharakati duniani kote kushiriki katika hashtag "#wewontbesilenced" (Hatutanyamazishwa).
0 Comments