Sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC iliyopata Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara, imemtibua kocha Abdelhak Benchikha aliyegeuka mbogo kwa wachezaji wa timu hiyo, kisha kuagiza usajili wa wachezaji wawili fasta kikosini ili mambo yawe mazuri.
Simba ililazimishwa sare hiyo kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam ukiwa ni mchezo wa pili kwa kocha huyo katika ligi tangu apewe mkataba kuinoa timu hiyo baada ya wenyeji KMC kuchomoa bao dakika chache kabla ya pambano hilo kumalizika baada ya Wazir Junior kutumia makosa ya kipa Ayoub Lakred.
Mara baada ya pambano hilo, kocha huyo aligeuka mbogo kwa wachezaji na fasta akawasiliana na mabosi wa klabu na unaposoma habari hii sasa tambua tayari Benchikha amewaambia mabosi wa juu kuwa, kabla ya kuingia mwaka mpya wa 2024 anataka haraka aletewe kiungo mkabaji wa maana ndani ya kikosi hicho. Mwanaspoti lilishawadokeza juu ya kiungo ambaye kocha huyo anamtamani ambaye ni Éric Mbangossoum kutoka Chad.
Benchikha anaona bado kuna shida kubwa eneo hilo la kiungo katika timu hiyo licha ya kuwa na mastaa kama Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma na Mzamiru Yasin na kiraka Kapama Nassor ambaye amekosa nafasi kikosi cha kwanza na sasa amesimamishwa sambamba na Clatous Chama kwa utovu wa nidhamu.
Kocha huyo anaamini tatizo la eneo hilo ndilo limeifanya Simba kupata shida mbele ya timu pinzani kwenye mechi inayozcheza ziwe za Ligi Kuu ama zile za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mbali na kiungo mkabaji pia kocha huyo ametaka kutafutiwa mshambuliaji wa kati mwenye ubora wa kutumia nafasi baada ya kuina jinsi timu yake inavyopoteza nafasi za mabao.
Benchikha amewaambia mabosi wa Simba, kwamba kama watapata mshambuliaji mtulivu anayejua kutumia nafasi kwa jinsi kikosi chake kinavyotengeneza nafasi za mabao anaweza kufunga mabao mengi yasiyopungua mawili hadi matatu kwa kila mechi. Katika mechi hiyo ya juzi, Benchikha aliwatumia nahodha John Bocco na Jean Baleke katika eneo hilo la mshambuliaji wa kati, huku Moses Phiri akiwa benchi na timu kushindwa kufanya maajabu mbele ya KMC.
Mara baada ya pambano hilo, Benchikha alisema akiwa na hasira; “Tunatengeneza nafasi nyingi lakini angalia tunavyokosa utulivu wa kuzitumia, hili ni tatizo kubwa hii ni sare ambayo tumezitengeneza wenyewe hasa wachezaji wangu.”
Tayari mabosi wa Simba wameshaingia sokoni kuanza msako huo wa mastaa hao wawili katika kuhakikisha wanaingia haraka ndani ya kikosi chao hicho.
“Kocha ameshasema kwamba anahitaji nafasi zipi tumemwambia yeye kama ana machaguo yake atuletee tutapima kwa pamoja na sisi kama wapo nas sisi tunawajua tutamletea haraka ili kusudi tufanye maamuzi kwa pamoja,” alisema bosi huyo wa juu wa Simba.
0 Comments