Angola ilitangaza jana Alhamisi kuwa inajiondoa katika kundi la wazalishaji wa mafuta la OPEC, baada ya kuzozana na kundi hilo kuhusu viwango vya chini vya uzalishaji mwaka huu.
Waziri wa Mafuta wa Angola, Diamantino de Azevedo, amesema kwamba nchi hiyo haifaidiki chochote kwa kubaki katika jumuiya hiyo na kwamba imechukua uamuzi wa kujiondoa kwenye OPEC.
Azevedo ameongeza kuwa: "Uamuzi huu ni wa nchi huru, daima tumefanya wajibu wetu lakini Angola imeamua kuondoka OPEC. Tunaamini kuwa wakati umefika kwa nchi yetu kuzingatia zaidi malengo yake."
Mzozo kuhusu kiwango cha chini cha uzalishaji wa mafuta kilichoainishwa kwa ajili ya baadhi ya nchi za Kiafrika, ikiwa ni pamoja na Angola, ulisababisha kucheleweshwa kwa siku nzima mkutano wa OPEC wa Novemba, ambapo kundi hilo, pamoja na wazalishaji washirika wakiongozwa na Russia, wanaamua ni kiasi gani cha mafuta kipelekwe masoko ya kimataifa ya bidhaa hiyo.
Angola na Nigeria ni wauzaji wakubwa wa mafuta katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika.
Wakati ikipoteza Angola, OPEC ilitangaza katika mkutano wake mwezi uliopita kuwa inaijumuisha Brazil katika kundi, nchi ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta na imekuwa ikizalisha kiasi kikubwa cha mafuta ghafi mwaka huu, kulingana na Wakala wa Kimataifa wa Nishati.
0 Comments