HATI ya makubaliano ya ushirikiano wa masuala ya kazi na ajira yaliyoingiwa kati ya Tanzania na Saudi Arabia imeanza kuzaa matunda baada ya Saudi Arabia kutoa nafasi 500 za ajira kwa wauguzi wa kike nchini.
Akitangaza nafasi hizo Dar es Salaam, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Cyprian Luhemeja alisema kuwa nafasi hizo ni kwa ajili ya wauguzi wa kike wa Kitanzania wenye elimu ya Stashahada na Shahada.
Luhemeja alisema nafasi hizo ni matunda ya hati ya makubaliano ya ushirikiano wa masuala ya kazi na ajira ulioingiwa kati ya Tanzania na Saudi Arabia ambayo yalisimamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Alisema Watanzania wenye ujuzi na sifa zilizobainishwa wanatakiwa kuomba kwa kujisajili kupitia https://jobs.kazi.go.tz pamoja na kutuma wasifu binafsi kwa njia ya barua pepe ya esu@taesa.go.tz hadi kufikia Desemba 31, 2023.
Luhemeja alisema mchakato wa kuwapata wauguzi hao unatakiwa kukamilika ifikapo Januari 10, 2024, hivyo waombaji wajitahidi kukimbizana na muda. Alisema kutokana na ufinyu wa muda tayari amekiagiza Kitengo cha huduma za ajira (TaESA) kuhakikisha kuwa hadi kufikia Januari 10 wote wenye sifa wawe wamepatikana kabla ya kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako.
Aidha, alisema wamepokea maelekezo kutoka kwa Rais Samia ya kuharakisha mazungumzo yanayoendelea kwa ajili ya uingiaji mikataba na nchi zingine 10 ili kuwapatia Watanzania fursa za ajira nje ya nchi. Alisema kuwa lengo la Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo yanakamilika ndani ya Januari 2024 na kuwataka Watanzania wanaotamani kufanya kazi nje ya nchi katika fani mbalimbali.
0 Comments