Gaza. Wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas imesema shambulizi la anga la Israel limeua takriban watu 70 katika kambi ya wakimbizi ya Al-Maghazi katikati mwa ukanda huo.
Taarifa zimesema huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kutokana na idadi kubwa ya familia zinazoishi katika eneo hilo.
Majeruhi wengi wamekimbizwa kutoka Maghazi hadi Hospitali ya karibu ya Al-Aqsa huku nyuso za watoto zikiwa na damu na miili inayozagaa nje.
Wizara ya afya inasema nyumba tatu zilipigwa katika shambulio hilo leo Jumapili Desemba 25, 2023.
Kulingana na Msemaji wa Wizara ya Afya, Ashraf al-Qudra, makazi yenye watu wengi yaliharibiwa.
Mwanaume mmoja amesema amempoteza bintiye na wajukuu zake, akiongeza kuwa familia yake ilikimbia kutoka Kaskazini kwa usalama katikati mwa Gaza.
"Ukuta uliwaangukia. Waliishi kwenye ghorofa ya tatu ya jengo moja. Wajukuu zangu, binti yangu na mumewe, wote wamefariki,” amesema mwanaume huyo.
"Sote tunalengwa. Raia wanalengwa. Hakuna mahali salama. Walituambia tuondoke katika Jiji la Gaza - sasa tulikuja Gaza ya kati kufa," ameongeza.
Jeshi la Israel limeiambia BBC kuwa, limepokea ripoti za tukio katika kambi hiyo.
Kulingana na wizara ya afya, zaidi ya watu 20,000 wameuawa wengi wao wakiwa watoto na wanawake na 54,000 wamejeruhiwa huko Gaza tangu vita hiyo ianze Oktoba 7, 2023 wakati Hamas na vikundi vingine vya Palestina viliposhambulia Israeli, na kuua watu 1,200 na kuchukua mateka wapatao 240.
Jana Jumapili Desemba 24, 2025 Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alisema vita hivyo vimekuja kwa gharama kubwa sana kwa nchi yake.
Jeshi la Israel limesema zaidi ya wanajeshi 12 wameuawa huko Gaza tangu Ijumaa, na kufanya jumla ya mashambulizi ya ardhini yaliyoanzishwa baada ya Oktoba 7 kufikia 156.
Jumamosi ilikuwa moja ya siku mbaya zaidi lakini Netanyahu amesema hakuna namna nyingine ila kuendelea kupigana.
0 Comments