Zaidi ya watu watano wapoteza maisha na wengine 90 kukosa makazi baada ya kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa saba mkoani Arusha.
Mvua hiyo iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Jumatatu Novemba 13, 2023 kuanzia Saa moja usiku imepelekea baadhi ya mitaro, vivuko, madaraja, barabara na nyumba za watu kujaa maji.
Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Felician Mtahengerwa amesema kuwa amepata taarifa hizo na kamati ya maafa pamoja na ile ya ulinzi na usalama zimeanza ziara maalum ya kutembelea maeneo yote ya jiji kuainisha madhara ya mafuriko hayo.
"Madhara ni makubwa kwa kweli na tuko kwenye ziara kutembelea maeneo yote na kuainisha ili angalau waathirika wapate msaada ikiwemo kuopoa miili iliyosombwa na maji na iliyoko kwenye nyumba zilizojaa maji lakini pia kuangalia namna ya kuwasaidia wananchi kupata malazi na kuwahamisha wale walioko kwenye hatari zaidi," amesema.
Amesema maeneo yaliyoathirika zaidi na majanga hayo ni Kata ya Muriet, Terrat, Majengo, Elerai na eneo la kwa Mrombo ambayo yanasababishwa na maji mengi ya mvua yanayotoka Arumeru kuelekea huko.
"Mbali na mvua zetu lakini maji mengi yametoka Arumeru na hadi sasa madhara makubwa yako kata hizo, hivyo subiri hadi baadae tukikamilisha zoezi tutatoa taarifa kikubwa wananchi wawe watulivu, wasikivu, waaminifu pia utiifu katika zoezi hili tunalolifanya," amesema DC Mtahengerwa.
Akizungumzia madhara hayo, Diwani wa Kata ya Muriet, Francis Mbise amesema kuwa katika kata yake miili mitatu imeshaopolewa kwenye mitaro na nyumba 23 zimepata madhara mbalimbali ikiwemo kuingiliwa maji na kubomoka ukuta ikiwemo maduka, hali iliyopelekea vitu kusombwa na maji.
"Kusema madhara hasa bado ni mapema maana ndio kwanza pamekucha na tumeshapata miili mitatu ambayo hatujawajua bado maana walikuwa ni wapita njia, na baadhi ya nyumba zimeezuliwa na kuanguka ukuta, hivyo vifo vya huko ndani kwenye majumba hatujajua zaidi ya hawa waliopatikana ni wapita njia," amesema.
Diwani wa Kata ya Sokoni One, Michael Kivuyo amesema kuwa madhara ya mafuriko hayo mbali na mwili wa mtu mmoja kuokotwa eneo la Lolovono bado hawajapa idadi kamili kutokana na mti mkubwa kuziba daraja la kuelekea makazi ya watu.
"Madhara ni makubwa, barabara zimemeguka, madaraja yamejaa maji na vivuko havifai, hofu kubwa ni baadhi ya nyumba zilizojaa maji kama wahusika wamenusurika hasa watoto hivyo tunatafuta msaada ya kuondoa miti iliyoziba daraja la Uswahili tukaone hali ikoje huko kwenye makazi," amesema.
Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita alisema kuwa athari zilizobainika hadi sasa ni nyumba kuporomoka na kuangukia kuta na maduka kuvunjika ambayo ni zaidi ya 25 na vitu kusombwa na maji vikiwemo vibanda vya matund, mbogamboga lakini vyombo vya moto hasa boda boda waliokuwa wanadharau wingi wa maji.
"Saa hizi bado asubuhi na ndiyo kwanza tumeamka kujua hali halisi, ni ngumu ila mvua kuanza mapema ilisaidia watu wakawa hawajalala, kwa hiyo waliodhurika wengi ni wale waliokuwa wanarejea makwao ndio wakapata ajali hizo hivyo pia tunamshukuru Mungu kwa hilo maana ingekuwa usiku wa manane tungekuwa na habari mbaya zaidi," amesema.
Amesema kuwa kwa kata yake baadhi ya vivuko vimekatika huku daraja kubwa la 'Kambi ya Fisi' kuvunjika na kukatisha mawasiliano kati ya Kata ya Ngarenaro na Sakina.
Mmoja wa wananchi jijini Arusha, Rehema Swai alisema kuwa hofu nyingine ni baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne ambao walistahili kufanya mitihani leo kuwa katika wakati mgumu kufanikisha zoezi hilo.
"Tunaomba Serikali ikiwezekana kuwasiadia kuwapa mtihani wa siri baadaye hawa ambao wananusuru maisha yao na kukosa mitihani," amesema.
Neema Laizer mkazi wa Kwa Morombo amesema kuwa mvua hiyo iliyoanza kwa kasi saa moja usiku imeezua nyumba za watu zaidi ya 30, kusomba vyombo vya moto na pia bidhaa mbalimbali madukani.
"Unajua hii mvua ilianza kama utani, tukadhani itakuwa kama ya siku zote lakini kadri muda ulivyokuwa inakwenda ndio mafuriko yakazidi yakaanza kusomba vitu vyote katika soko letu 'Kwa Morombo' madukani yakaingia, na magari na majaji pia pikipiki zikaanza kupoteza uelekeo na kuingia kwenye mitaro," amesema.
0 Comments