Makahaba wamekiri kupitia hali ngumu kiuchumi, ikibainika kuwa siku hizi wanagombania wateja na baadhi ya akina mama fua (wanawake wanaokwenda kwenye miji za watu kutafuta kazi za kufua nguo).
Kwa upande mwingine, ni hali ambayo imekuwa ikiwakosesha usingizi huku akina mama fua wakivuna pakubwa.
Ikumbukwe kuwa mama fua hutoa huduma zao kwa kuzunguka kutoka nyumba moja hadi nyingine, lakini makahaba huwinda wateja kwenye kona zilizofichika na vituo maarufu vya kibiashara nchini kama vile Salgaa, Kikopey, Maai Mahiu na Mlolongo.
Upekuzi wa Taifa Leo Dijitali unaonyesha kuwa wanaume wengi siku hizi wanapendelea huduma za akina mama fua kwa kile wanachodai “ni wachapakazi”.
“Hakuna wafanyikazi wenye bidii kama mama fua kwa sababu wana tabia nzuri, moyo safi na wanaojitolea,” anasema Kennedy Keitany mkazi Nakuru.
Keitany anasema ingawa kuna watu ambao wanawaelewa vibaya wakidhani wanaleta ushindani mkali katika sekta ya ukahaba.
Irene Mwende, mama fua kutoka eneo la Uthiru, Kaunt ya Kiambu anasema anajivunia kazi yake kwa sababu ndiyo humpatia riziki ya kila siku. Anasema makahaba wa siku hizi ni wezi, na kwamba hawana ujuzi kubembeleza wateja.
“Wanajulikana kwa kuwekea wateja mchele kwenye vinywaji nia yao kuu ikiwa ni kuwapora, kinyume na akina mama fua ambao kazi yao ni kufua, kusafisha nyumba na mara nyingine hutoa huduma za masaji,” akasema.
Mwende anasema ukizuru kituo cha Salgaa jijini Nakuru utashangaa kuwaona makahaba wa kila rika wakitafuna mogoka na hata mara nyingine kuvuta bangi waziwazi.
Anasema ikiwa ni watu wema, basi kwa nini wanapenda kujificha gizani na kuendesha biashara za usiku tu?
Mwende amewataka watu kutupilia mbali dhana kwamba baadhi ya akina mama fua huwa wamejificha ndani ya ngozi ya kondoo kwa kuhubiri maji na kunywa divai.
Bi Irene (sio jina halisi) kahaba kutoka mtaa wa Eastleigh 12th Street, anasema biashara ya ukahaba inalipa ila wanapitia changamoto tangu akina mama fua wajitose uwanjani.
“Wakati mwingine kina mama fua hutundika picha mtandaoni wakiwa wamevalia mavazi ambayo kwa kawaida hayana tofauti kubwa na yale yanayovaliwa na makahaba wenzetu,” anasema.
Anasema na kwenye mitandao ya kijamii kuna makundi mengi ya mama fua, ambayo huambatana na huduma za ziada almaarufu extras.
Huduma za ziada katika kisa hiki, ni kuwapa mahaba waseja – wanaume ambao hawajaoa, hasa baada ya kufuliwa nguo.
0 Comments