Mufti Zubeir ataka watoto wasomeshwe badala ya kulalamikia ajira

 Arusha. Sheikh Mkuu Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir ametaka wazazi na walezi nchini kusomesha watoto elimu ya dini na dunia, ili waweze kupambana vizuri katika soko la ajira badala ya kubaki kuwa walalamikaji.



Kumekuwepo na changamoto ya ajira kwa vijana kutokana na uwepo wa fursa chache za kuajiriwa katika sekta za umma na binafsi na licha ya kuhitimu elimu katika vyuo mbalimbali.


Akizungumza katika maadhimisho ya Maulid ya Kuzaliwa Mtume Mohamed SAW jijini Arusha leo, Mufti Abubakar Zubery amesema wakati wa kulalamika umepita na sasa jitihada zinapaswa kuongezwa katika elimu.


"Somesheni watoto wenu elimu zote ili waweze kuwa na sifa na maarifa ya kuajiriwa na kujiajiri badala ya kuendelea na kulaumu kuwa tunaonewa,"amesema.


Amesema hakuna sehemu ambayo wataweza kuajiri kijana ambaye hana sifa hivyo ni lazima kusoma kama ambavyo dini ya Kiislamu ilivyoelekeza.


Amesema pia Waislamu nchini lazima waingie katika biashara na kuwekeza katika sehemu mbalimbali ili kujipatia vipato vya kuboresha uchumi wao na Taifa.


Awali, Sheikh Mkuu wa Mkoa Arusha, Sheikh Shaban Juma amesema dhana ya kutetea haki za binaadamu duniani isiwe ni kigezo cha kuvuruga maadili na utulivu katika jamii.


Sheikh Juma amewataka watanzania kuwa makini na mambo ambayo yanaletwa hivi kwa lengo madai ya ukombozi wa watu kwani baadhi yanakinzani na dini, mila na utamaduni wa Mtanzania.


"Pia kuna hili suala la haki za wanawake ni muhimu ifahamike kuwa Waislamu wanalinda haki hizo, ikiwepo kutambua haki za wanawake kurithi mali,"amesema.


Mbunge wa Jimbo la Arusha, Mrisho Gambo amesema Waislamu Mkoa Arusha wanapongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia kuwapatia Waislamu eneo lililopo mbele ya Msikiti Mkuu wa Arusha.


Amesema mikakati imeanza eneo hilo kujengwa vizuri na kutumika kama kitega uchumi lakini pia kutoa huduma kadhaa kwa Waislamu na kwa Wakazi wa Jiji la Arusha.


"Mheshimiwa Sheikh Mkuu tutakapokuja kwao kuhusu kuweka alama ya mradi katika eneo hili tutaomba ushirikiano wako," amesema.


Amesema aliomba Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) Mkoa Arusha kufanya mashindano kwa madrasa zote katika Jiji la Arusha ili kutambua vipaji vya wanafunzi wanaofanya vizuri na waweze kupewa zawadi.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE