Bukombe. Watu sita wamefariki na wengine wawili kujeruhiwa baada ya gari ya abiria kugongana uso kwa uso na lori katika eneo la Mzibira kata ya Uyovu wilayani Bukombe Mkoa wa Geita.
Akithibitisha ajali hiyo, Kamada wa Polisi Mkoa wa Geita, Sofia Jongo amesema tukio hilo limetokea leo saa 12:07 alfajiri katika eneo la Mzibira wilayani Bukombe na kudai licha ya dereva wa gari iliyokuwa imebeba abiria (Haice) kuwa mwendokasi lakini pia alisinzia.
Kamada Jongo amesema gari hiyo ya abiria iliyokuwa inatokea wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga kwenda Nyakanazi wilayani Biharamulo imegongana uso kwa uso na lori hilo lililokuwa linatoka Nyakanazi kwenda Kahama huku dereva wa gari dogo na kondakta wake wakifariki pamoja na abiria wengine wanne.
"Ni kweli tukio hilo lipo na hapa natoka eneo la tukio wamekufa watu sita kati yao ambao ni dereva, kondakta na abiria wanne waliokuwa kwenye gari dogo, majeruhi wawili wamekimbizwa hosipitali ya Uyovu na kwa sasa tunavyoongea wamepewa rufaa ya kwenda hospitali ya Mkoa Geita kutokana na hali zao kutokuwa nzuri,” amesema Jongo
Jongo ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari wakati wote wanapokuwa wanaendesha ili kuepusha ajali zisizo za lazima na kugharimu maisha ya Watanzania.
Naye shuhuda wa tukio hilo, John Kulinda amesema eneo hilo limekuwa na ajali za mara kwa mara kwani wiki mbili zilizopita mwendesha pikipiki (bodaboda) aliyekuwa na abiria wawili akiwamo mtoto walipoteza maisha kwenye ajali katika eneo hilo, ambapo ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kudhibiti ajali hizo kwa kuweka tuta.
“Nilifika hapa (eneo la ajali) saa 12:55 asubuhi nikiwa na abiria wangu nilikutana na ajali hiyo nilianza kuona mili ya watu wawili waliofariki badaye nikaona miili mingine imelala chini roho imeniuma sana sikufanya chochote niliamua kuondoka,” amesema Kulinda
Diwani wa kata ya Uyovu, Kulusanga Inyasa ameiomba Serikali ichukue hatua ya kujenga tuta eneo hilo na kuzuia mwendo kasi pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto ili wajue athari za ajali.
0 Comments