Katika hali isiyo ya kawaida wanafunzi wa Kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya wasichana Loleza (Mchepuo wa HGL) usiku wa kuamkia Julai 11, 2023 walilazimika kulala darasani ikidaiwa kuwa ni baada ya mwalimu wa bwenini kuondoka na funguo za bwenini kwao.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera kupitia vyanzo vyake vya taarifa anasema alipata taarifa za tukio hilo na kuamua kufanya ziara ya kushtukiza shuleni hapo.
Homera ameeleza kukerwa na tukio hilo kwenye shule ya Loleza anayosema ni ya mfano ikikusanya watoto kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini hivyo hata kama watoto walifanya kosa ilifaa kupewa adhabu walizojiwekea shuleni hapo na si kuwalaza darasani ikizingatiwa na musimu huu wa baridi.
Mwalimu anayedaiwa kuondoka na funguo za bweni ambaye ni msimamizi wa watoto hao bwenini Sabina Haule anasema chanzo ni ukorofi wa watoto hao lakini hakuwaamuru kwenda kulala darasani kwa kuwa baada ya kufunga bweni alirudi baadaye majira ya saa nne usiku na kuwaelekeza kwenda kulala mabweni mengine ambayo hayana wanafunzi lakini watoto hao walikaidi na kwenda kulala darasani kimyakimya hivyo kuomba msamaha kwa mkuu wa mkoa.
Mkuu wa Shule ya Loleza Mwalimu mkuu Betiseba Nsemwa alipoulizwa juu ya suala hilo amesema alikuwa akiendelea kushughulikia suala hilo kwa kuwakutanisha mwalimu wa nidhamu na msimamizi huyo wa bweni.
Baadaye mkuu wa mkoa Juma Zubery Homera akapata nafasi ya kutembelea hadi darasa ambalo wanafunzi wanadaiwa kulala usiku mzima kisha kuzungumza na wanafunzi hao akiwaasa kuzingatia nidhamu wawapo masomoni na kumuagiza afisa elimu mkoa Mwalimu Ernest Hinjo kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mwalimu husika.
0 Comments