Arusha. Sintofahamu imeibuka jijini Arusha, baada ya Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita kusitisha mkutano wa Injili wa Mhubiri Ezekiel Odero ambaye ametajwa kuwa na ‘ushirika’ na Mchungaji ‘tata’ Paul Mackenzie, anayedaiwa kusababisha vifo vya waumini wake zaidi ya 300 nchini Kenya.
Akizungumza na mwananchi Leo Julai 14, 2023 diwani huyo amesema amepokea maelezo ya kusitishwa mkutano huo.
"Afisa Utamaduni wa Jiji alitoa kibali bila kufanya mashauriano na sisi kama viongozi wa Kata na viongozi wake wa juu kwani ule uwanja upo shuleni na wanafunzi wapo kwenye mitihani," amesema.
Doita amesema, ambacho amefanya leo ni kuomba kupunguzwa sauti kwani ni kero kwa wanafunzi wakati vyombo vingine vikiendelea na kusitisha mkutano.
Hata hivyo leo wakati maelfu ya watu wakiwa tayari wamewasiri uwanjani huku wakiendekea na maombi juu ya Jiji la Arusha, Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya Arusha imeamua kusitisha kibali hicho.
Mhubiri huyo akishirikiana na Mtanzania Soni Nabii walikuwa waanze mkutano wa siku tatu katika viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro, ambao upo jirani Sekondari ya Ngarenaro.
Muhubiri Odero aliwahi kutajwa kuwa ni mshirika wa Mackenzie ambaye anatuhumiwa kusababisha vifo vya waumini wake zaidi ya 300 kati ya mwezi Machi na June, kutokana na mafundisho yake, ambapo inadaiwa aliwataka waumini hao wafunge hadi kufa ili wakutane na Mungu.
Miili ya waumini hao ilibainika na polisi wa Kenya baada ya zoezi la kutafuta na kufukua makaburi ya halaiki katika Msitu wa Shakahola, uliopo karibu na mji wa pwani wa Malindi, ambapo waathiriwa wa kwanza baadhi yao walifariki na wengine kukutwa hai lakini wakidhoofika kiafya.
Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Lucy Kilanga, jana alikiri kutoa kibali hicho cha kufanyika mkutano wa injili wa siku tatu katika viwanja vya Shule ya Ngarenaro.
"Wewe jua kibali kimetolewa wafanye mkutano wa injili basi hayo mengine wewe yanakuhusu nini?" amehoji afisa kisha kukata simu.
Hata hivyo Mchungaji Odero ambaye anatokea Kanisa la New Church la Kenya, jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari, amekana kuwa na uhusiano na Mchungaji Mackenzie, na hivyo akawataka watu kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo.
Mmoja wa waumini wake, Julius Nkya akizungumza na Mwananchi uwanjani hapo amesema kilichotokea Kenya ni chuki za kisiasa baada ya Mchungaji Odero kutojihusisha na kuchangia wagombea.
"Ndio sababu baada ya uchunguzi aliachiwa, sasa mimi ni muumini wake miaka mingi ndio sababu nimefika hapa," amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha Justine Masejo amesema Jeshi hilo linafuatilia mgogoro wa uwepo wa mhubiri hayo.
0 Comments