Hai. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Hai, Itikija Msuya ametakiwa kumsaka muuguzi wa hospitali ya wilaya aliyekataa kumchoma sindano mgonjwa kwa madai ya kukataa kununua dawa zake.
Agizo hili limetolewa Juzi na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Amir Mkalipa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano mkuu wa halmashauri hiyo.
Mkalipa alisema awali, mgonjwa huyo aliandikiwa dawa na daktari, lakini muuguzi huyo akamwambia anazo dawa zake na asiende kununua pengine.
Alisema jambo hilo mgonjwa alilitilia shaka na kumkatalia.
“Huyu mgonjwa aliandikiwa dawa na daktari, sasa nesi aliyekuwa akimhudumia akamwambia usiende kununua hiyo dawa mimi ninayo, leta fedha nikuchome sindano, yule mgonjwa akakataa, akaenda kununua dawa, aliporudi akamwambia hii hapa nichome, yule nesi akakataa kumchoma,” alisema Mkalipa.
“Sasa huyu mgonjwa aliyekataliwa kuchomwa sindano akaja ofisini kwangu kuniletea malalamiko, nikaagiza apigiwe simu hakupatikana, sasa DMO nakuagiza nataka umtafute kwanza huyo nesi tumjue alafu tutaongea.”
Alisema kufuatia malalamiko kuwa mengi aliahidi kwenda hospitalini hapo kuzungumza na watumishi wote wa hospitali hiyo ili kufahamu kwa nini wanatoa lugha chafu kwa wagonjwa pamoja na kutoa huduma zisizoridhisha.
“Mimi nitakwenda kukaa na watumishi wa afya ili tukubaliane namna ya kufanya kazi na kama kuna mtu amechoka kufanya kazi mjini basi tutampeleka huku kwingine akafanye kazi, DMO ongea na ofisa tawala amtafute huyo nesi aliyekataa kumchoma sindano mgonjwa aliyeandikiwa dawa na daktari,” alisema.
Hata hivyo, mganga mkuu wa wilaya aliahidi kuyafanyia kazi maagizo hayo akisema huduma za upatikanaji wa sasa katika hospitali ni zaidi ya asilimia 93.
“Mkuu nimepokea maelekezo yako ya kumtafuta nesi aliyemhudumia huyo mgonjwa na nakuahidi nitaifuatilia kwa hatua zaidi,” alisema Dk Msuya.
0 Comments