18 wajeruhiwa ajali ya Coaster Same

 

Same. Watu 18 wamejeruhiwa wilayani Same mkoani Kilimanjaro baada ya basi aina ya Coaster walilokuwa wamepanda kutoka Dar es salaam kuja Kilimanjaro kutumbukia kwenye korongo katika eneo la Mabilioni mpakani mwa wilaya za Korogwe na Same huku dereva wa gari hilo akidaiwa kuwa alisinzia.



 Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema imetokea leo Julai 14, 2023 saa 10 alfajiri ambapo dereva pamoja na abiria waliokuwepo kwenye gari hilo walikuwa wamesnzia.


Kasilda amesema baadhi ya majeruhi hao wamevunjika mikono, wamejeruhiwa kichwani na sehemu za mbavu ma kati ya majeruhi hao, 10 wamekimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) baada ya hali zao kuwa mbaya huku wengine walipatiwa huduma katika kituo cha afya cha Hedaru na hospitali ya wilaya ya Same.


“Ni kweli kumetokea ajali alfajiri ya leo kati ya majira ya saa 9 au 10 usiku katika eneo la Mabilioni karibu na mpaka wa Korogwe na Same, inavyoonekana ni kama dereva alisinzia,” amesema.


Mkuu huyo wa wilaya amesema kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, abiria wote walikuwa wamelala na hadi ajali inatokea, walikuwa hawajui kilichotokea mpaka hapo walipookolewa kwenye korongo hilo ambalo ni mkondo wa maji.


“Idadi ya abiria waliokuwa kwenye Coaster ni 25 lakini waliojeruhiwa ni 18, wawili ambao hawakujeruhiwa sana walikimbizwa kituo cha afya cha Hedaru wanaendelea na matibabu pale, lakini 16 walipelekwa hospitali ya wilaya ya Same kwa sababu walikuwa wamejeruhiwa sana na kati ya hawa, 10 walikimbizwa hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi.


“Majeruhi wengi walipata majeraha kichwani, kwenye mbavu, wengine wamevunjika mikono, bahati mbaya walikaa muda mrefu pale kwa sababu ni eneo ambalo halina nyumba za kuishi ni mashamba tuu,” amesema.


Hata hivyo, Kasilda amesema baada ya kutokea ajali hiyo dereva wa gari hilo alitoroka kusikojulikana.

0 Comments

banner

Ahsante kwa kutembelea zotekali blog ili kuwa karibu nasi kila wakati Jiunge katika kurasa zetu zamitandao ya kijamii  facebook , Twitter, Instagram na Youtube  NI BUREE