Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Kilosa, Mhandisi Josh Chumu.
Aweso amemsimamisha Chumu kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kata ya Ruaha, ambao wamedai kuwa ameshindwa kusimamia vyema miradi ya maji katika Wilaya ya Kilosa na kusababisha kuchelewa kwa miradi, licha ya serikali kutenga fedha zaidi ya Shilingi bilioni 4 za utekelezaji wa miradi ya maji eneo la Ruaha na usimamizi mbovu wa jumuiya za watumia maji.
Ametoa uamuzi huo katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maji, ambapo baada ya kufika Jimbo la Mikumi alipokea malalamiko na kero nyingi kutoka kwa wananchi.
Wananchi hao walilamikia adha kubwa ya maji ya muda mrefu, licha ya maeneo yao kuzungukwa na vyanzo vingi vya maji, ikiwemo milima ya Udzungwa pamoja na mito.
Waziri Aweso pia amemtaka Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Morogoro awaombe radhi wananchi wa Wilaya ya Kilosa kwa kushindwa kusimamia vyema miradi ya maji iliyokuwa mkoani kwake na kutoa maelekezo mahususi kwa mkandarasi mradi wa Maji Ruaha ukamilike haraka iwezekanavyo na ndani ya mwezi Januari awe ametandaza mabomba.
0 Comments