KIAMSHA kinywa mara nyingi huitwa ‘mlo muhimu zaidi wa siku’.
Licha ya manufaa ya kifungua kinywa kwa afya na ustawi wako, watu wengi mara nyingi huruka au hukosa kwa sababu mbalimbali.
Habari njema ni kwamba kuna njia nyingi za kurahisisha kuweka kiamsha kinywa katika siku yako.
Umuhimu wa kiamsha kinywa
Nishati
Chanzo cha nishati ya mwili ni glukosi. Glukosi huvunjwa na kufyonzwa kutoka kwa chakula cha wanga ambacho mja hula. Mwili huhifadhi nishati yake nyingi kama mafuta. Lakini mwili wako pia huhifadhi glukosi kama glaikojeni nyingi kwenye ini lako, na viwango vidogo kwenye misuli yako. Wakati wa kutokula kama vile usiku, ini huvunja glaikojeni na kuitoa kwenye damu yako kama glukosi ili kuweka viwango vya sukari yako ya damu kuwa thabiti. Hii ni muhimu sana kwa ubongo wako, ambao unategemea glukosi kwa nishati. Asubuhi, glaikojeni huwa chini. Mara tu nishati yote inapotumika, mwili wako huanza kuvunja asidi ya mafuta ili kupata nishati inayohitajika. Lakini bila kabohaidreti, asidi ya mafuta ni sehemu tu ya oksidi, ambayo inaweza kupunguza viwango vya nishati yako.
Kula kiamsha kinywa huongeza viwango vyako vya nishati na kurejesha viwango vyako vya glaikojeni tayari kutumika kwa mifanyiko ya kimetaboliki.
Vitamini muhimu, madini na virutubisho
Vyakula vya staftahi vina virutubisho vingi muhimu kama vile folati, kalsiamu, chuma, vitamini B na nyuzi. Kiamsha kinywa hukupa kwa wingi virutubisho unavyohitaji wakati ukiendelea na shughuli za siku. Vitamini muhimu, madini na virutubisho vingine vinaweza kupatikana tu kutoka kwa chakula, kwa hivyo, ingawa mwili wako unaweza kupata nishati ya kutosha kwa mlo unaofuata, bado unahitaji kuongeza viwango vyako vya vitamini na madini ili kudumisha afya na uchangamfu.
Kiamsha kinywa husaidia kudhibiti uzito wako
Watu wanaokula kiamsha kinywa mara kwa mara wana uwezekano mdogo wa kuwa na uzito kupita kiasi. Kula kiamsha kinywa kunaweza kukusaidia kudhibiti uzito wako kwa sababu:
Huzuia mabadiliko makubwa katika viwango vya sukari ya damu, kukusaidia kudhibiti hamu yako ya kula.
Kifungua kinywa hukushibisha kabla ya kuwa na njaa sana, kwa hivyo kuna uwezekano mdogo wa kunyakua tu vyakula vyovyote vilivyo karibu wakati unapohisi njaa.
Kiamsha kinywa huongeza uwezo wa akili
Ikiwa huli chakula cha staftahi, unaweza kupata unahisi uchovu na kutokua makini. Hii ni kwa sababu ubongo wako haujapokea nishati inayohitajika. Kutokula kifungua kinywa huathiri utendaji wako wa kiakili, pamoja na umakini wako, uwezo wa kuzingatia na kumbukumbu.
Kifungua kinywa cha afya kinaweza kupunguza hatari ya magonjwa
Ikilinganishwa na watu ambao hawali kifungua kinywa, wale ambao hula kiamsha kinywa mara kwa mara huwa na hatari ndogo ya ugonjwa wa kunenepa sana na ugonjwa wa kisukari.
Kiamsha kinywa hukusaidia kufanya chaguo bora zaidi za chakula
Watu wanaokula kiamsha kinywa kwa ujumla huwa na lishe bora zaidi kwa ujumla, wana mazoea mazuri ya ulaji na wana uwezekano mdogo wa kuwa na njaa ya vitafunio wakati wa mchana kuliko watu ambao wanaruka kifungua kinywa.
Hili linaweza kuwa tatizo ikiwa vitafunio hivyo vina nyuzinyuzi kidogo, vitamini na madini, vyenye mafuta mengi na chumvi nyingi. Bila nishati ya ziada ambayo kifungua kinywa kinaweza kutoa, baadhi ya watu huhisi uchovu na kugeukia vyakula na vinywaji vyenye nishati nyingi.
Ukikosa kifungua kinywa, jaribu vitafunio vyenye wingi wa madini, vitamini na virutubisho vingine kama vile matunda au mtindi ili kukusaidia kukabiliana na njaa.
0 Comments