Shirikisho la soka nchini Iran limeilalamikia Fifa baada ya nembo ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kuondolewa kwenye bendera yake katika mitandao ya kijamii na timu ya Marekani.
Kabla ya mkutano wao wa Kombe la Dunia siku ya Jumanne, Marekani iliondoa alama ya Allah katika picha zilizochapishwa kwenye Twitter, Facebook na Instagram.
Marekani ilisema iliamua kutotumia bendera rasmi ya Iran kuonyesha "uungaji mkono kwa wanawake nchini Iran wanaopigania haki za kimsingi za binadamu", huku kukiwa na maandamano makubwa ya kuipinga serikali nchini humo.
Maandamano nchini Iran, yalikabiliwa na msako mkali, yamechochewa na kifo cha Mahsa Amini, aliyefariki akiwa kizuizini mwezi Septemba, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 ambaye alizuiliwa na polisi wa maadili kwa madai ya kuvunja sheria kali za kufunika kichwa.
"Katika kitendo kisicho cha kitaalamu, ukurasa wa Instagram wa shirikisho la soka la Marekani uliondoa nembo ya Allah kwenye bendera ya Iran," lilisema shirika la habari la Iran IRNA.
"Shirikisho la Soka la Iran lilituma barua pepe kwa Fifa (shirika linalosimamia soka duniani) kutaka itoe onyo kali kwa shirikisho la Marekani."
Msemaji wa Soka la Marekani baadaye alisema ujumbe huo umeondolewa na kuwekwa mwingine wenye bendera sahihi ya Iran, lakini akaongeza: "Bado tunaunga mkono wanawake wa Iran. "
Iran imeishutumu Marekani na wapinzani wengine wa kigeni kwa kuchochea maandamano hayo, huku serikali ya Marekani ikiwawekea vikwazo maafisa wa Iran kutokana na ukandamizaji huo.
Marekani na Iran zilikata uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1980.
0 Comments