Kamati ya pamoja ya ununuzi wa pembejeo za zao la korosho na wazabuni wamesaini mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 375.5 kwa ajili ya ununuzi na usambaji wa pembejeo hizo kwa msimu wa mwaka 2023/2024.
Zoezi hilo la utiaji saini limefanyika leo, Jumamosi, mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas ambaye ameitaka kamati hiyo na Bodi ya Korosho kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa mikataba kama ambavyo wamekubaliana.
Amesema amezitaka pande hizo mbili kuhakikisha kuwa hawamwonei huruma wazabuni hao na iwapo watashindwa kutekeleza mikataba hiyo kwa wakati wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
“Kumekuwa na hulka ya wazabuni kutoa visingizio mbalimbali kunapotokea ucheleweshaji na kamati imekuwa ikikubaliana nao, jambo hilo mwisho wake linaathiri zao la korosho.
“Serikali haitavumilia aina yoyote ya ucheleweshaji wa pembejeo, niwaombe Vyama Vikuu pamoja na Bodi ya Korosho kutekeleza majukumu yenu kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu,” amesema
Kwa mujibu wa Katibu wa Kamati hiyo Mohamedi Nassoro, mikataba hiyo ni ya kuagiza salfa ya unga tani 70,000 kwa ajili ya kukinga ubwiriunga, kiuatilifu kwa ajili ya ugonjwa wa Chule tani 200, na kiuatilifu kwa ajili ya Mbu wa Mikorosho na Minazi lita 600,000.
Viutilifu vingine ni lita 100,000 kwa ajili ya ubwiriunga pekee, lita 200,000 kwa ajili ya vidung’ata, lita 1,800,000 kwa ajili ya kutibu blaiti na lita 500,0000 kutibu ubwirirunga.
Aidha wazabuni hao wamepewa jukumu la kuagiza magunia million 6,700,000 na mabomba ya kupulizia elfu 6,500.
Serikali imeendelea kuweka jitihada kwenye kilimo cha korosho ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili ifikie tani 700,000 ifikapo mwaka wa fedha wa 2025/2026.
0 Comments